Wednesday, September 30, 2009

HUYU NDIYE DK SALIM AHMED SALIM







Dk Salim: WanaCCM waachwe
wapambane na Kikwete 2010

ASEMA MFUMO WA SERIKALI UMEOZA KWA RUSHWA

Elias Msuya

MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM na waziri mkuu wa zamani, Dk Salim Ahmed Salim amesema kuwa wanachama wa chama hicho wanaotaka kugombea urais sambamba na Jakaya Kikwete waachwe wapambane naye, lakini akasema hawatamuweza.

Baadhi ya jumuiya za CCM na vikundi kadhaa ndani ya chama hicho vimeshamtangaza Kikwete kuwa mwanachama mwingine asijitokeze kupambana na Kikwete kwenye uchaguzi ujao na kwamba vinamuunga mkono kiongozi huyo.

Lakini Dk Salim, ambaye aliwahi kuwa katibu mkuu wa Umoja wa Afrika (OAU), aliiambia Mwananchi katika mahojiano maalum nyumbani kwake jijini Dar es Salaam jana, WanaCCM wana haki ya kupambana naye kuwania kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho tawala..

Dk Salim alisema si makosa kwa wanachma wa CCM kujitokeza kuomba ridhaa ya wanachama kugombea urais kwa tiketi ya CCM katika kipindi cha kwanza cha rais aliye madarakani.

Alisema kwamba licha ya kuwepo kwa utaratibu wa CCM wa kumuachia rais aliye madarakani amalizie vipindi viwili vya madaraka yake, bado haoni tatizo kwa mwanachama wa chama hicho kujitokeza kugombea urais.

Alisema kwamba hata kama wanachama hao watajitokeza watapitia kwenye taratibu na mchakato wa chama wa kuwachuja.

"Huo ni utaratibu wa CCM ambao una maslahi kwa chama. Hata hivyo, watu wanaweza kujitokeza tu kugombea sambamba na Rais Kikwete. Kama watajitokeza watapitia kwenye mchakato wa chama ambacho ndicho kitaamua kimpitishe nani. Hata hivyo, kwa sasa sioni mtu wa kumshinda Rais Kikwete," Dk Salim alisema.

“CCM ina utaratibu wa kuachiana vipindi viwili. Ni utaratibu uliowekwa kwa maslahi ya chama katika mazingira ya siasa za leo. Lakini, hata kama watajiotokeza wanachama wengine, bado Rais Kikwete ana nguvu ya kuwashinda. Sidhani kama kuna mwanachama ambaye anaweza kupitishwa zaidi ya Kikwete,”.

Hadi sasa mbunge wa jimbo la Maswa mkoani Shinyanga, John Shibuda ndiye pekee aliyetangaza nia yake ya kuvaana na Kikwete kuomba ridhaa ya chama kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2010.

Makamu mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa alishaweka wazi kwamba katika mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia chama hicho mwakani ni ruksa kwa wanachama kuomba nafasi ya urais kwa kuwa katiba inawaruhusu.

Lakini kabla ya Msekwa kutoa ufafanuzi huo, makamu mwenyekiti wa zamani wa CCM, John Samuel Malecela, kundi la wenyeviti wa mikoa na wazee wa chama hicho, walitangaza wazi kwamba Rais Kikwete apitishwe amalizie kipindi chake cha pili cha uongozi kama ilivyo desturi ya chama hicho.

Mfumo wa serikali unanuka rushwa

Akizungumzia suala la mapambano ya rushwa, Dk Salim alisema mfumo wa serikali ya Tanzania umeoza kwa rushwa na hivyo hauwezi kumsaidia rais kuikabili, hivyo rushwa kutawala kuliko kitu kingine.

Alisema tofauti na wakati wa rais wa awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Nyerere wakati rushwa ilipodhibitiwa kikamilifu, wakati huu rushwa imeachiwa nafasi kubwa kiasi ambacho kinafanya hali ya Watanzania kudorora.

“Tukisema kwamba tatizo halipo tutakuwa tunakosea. Tulilokosea ni kuliachia tatizo la rushwa lishamiri kama lilivyoshamiri sasa. Rushwa haikuanza jana, haikuanza na serikali ya awamu ya nne, wala serikali ya awamu ya tatu wala ya pili. Rushwa ilikuwepo tangu awamu ya kwanza," alisema.

Lakini akasema tofauti kubwa kati ya awamu hizo na ile ya Mwalimu Nyerere ni kwamba muasisi huyo wa taifa alionyesha kwa vitendo kuwa rushwa ni jambo aliloamua kulifungia mkanda na kupambana nalo, lakini baada ya hapo tatizo hilo limeachiwa liendelee kiasi cha rushwa kugeuka kuwa utaratibu.

Alisema kwamba licha ya nia njema ya Rais Kikwete ya kupambana na rushwa na ufisadi, bado mfumo mzima wa serikali umeoza kiasi ambacho haiwezekani kupambana na rushwa.

“Rais Kikwete anajitahidi na ana nia ya kupambana na rushwa, lakini bado 'system' (mfumo) haijajitayarisha vya kutosha kupambana rushwa,” alisema.

Licha ya kuitetea CCM kuwa haihusiki na ufisadi bali baadhi ya watendaji wake ndiyo wanaojihusisha na ufisadi, Dk Salim alisema rushwa ni kansa inayoitafuna nchi.

“CCM kama chama si tatizo bali baadhi ya viongozi hawafuati katiba ya chama. Rushwa ni kansa inayoathiri jamii ya Watanzania. Mategemeo ya wananchi ni kuona CCM ndiyo iwe mstari wa mbele kupambana na rushwa na ufisadi kwa sababu hata katiba na ahadi za chama zinasema rushwa ni adui, sitapokea wala kutoa rushwa. Sasa hapa ndiyo kwenye tatizo,” alisema Salim.

Aupongeza uongozi wa Spika Sitta

Dk Salim alisema kwamba Bunge la sasa limepiga hatua kubwa katika kutoa kero za wananchi hasa kipindi hiki cha mfumo wa vyama vingi.

“Kwa kweli Spika Samuel Sitta amejitahidi sana kuendesha Bunge lenye viwango, hasa wakati huu wa mfumo wa vyama vingi. Bunge ndiyo sauti ya wananchi; ni njia pekee ya wananchi kutoa kero zao kwa serikali. Kwa hiyo linatakiwa liendeshwe katika 'health environment' (mazingira mazuri),” alisema.
“Tukiwa na Bunge kama hili ambalo linawapa wabunge nafasi ya kuzungumza kama hivi ni safi kwani inakuwa changamoto kwa mawaziri. Inawalazimu mawaziri kuwa na 'home work '(kazi ya ziada) kila wanapokwenda bungeni kujibu maswali" alisema Salim.

No comments:

Post a Comment