Tuesday, July 2, 2013

OBAMA TANZANIA

Ziara ya Obama Ni ujio wa neema au mashindano ya rasilimali? Elias Msuya Wakati Rais wa Marekani, Barrack Obama akizuru nchini, kumekuwa na hisia tofauti miongoni mwa wachambuzi wa masuala ya maendeleo ya jamii na uchumi. Akizungumza baada ya kuwasili nchini, Rais Obama anasema kuwa ziara yake imelenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kwa maslahi ya Marekani na Afrika. “Tunachofanya ni kuongeza bidhaa tutakazozalisha na kuangalia vyanzo vya asili na vya kawaida. Ninachotaka kusema na nimekuwa nikisema katika ziara yangu Afrika, sasa tunaangalia si tu kutoa misaada bali kufanya ushirikiano wa kibiashara. Kila tunapotoa fedha au dawa ni muhimu tujenge miundombinu ya afya itakayosaidia Tanzania,” anasema Obama. Naye mwenyeji wake Rais Jakaya Kikwete akizungumza katika mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) ametetea ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani akisema kuwa umesaidia kukuza uchumi wake na Afrika kwa ujumla. “Tunashirikiana na Marekani katika miradi mbalimbali na moja ya miradi mikubwa inagharimu kiasi cha dola 700 milioni. Kuna miradi mikubwa kama vile Pepfa inayogharimia mapambano ya malaria.” Akizungumzia ushindani kati ya mataifa ya Marekani na China katika miradi ya maendeleo nchini, Rais Kikwete anasema kuwa misaada ya Marekani imekuwepo hata kabla ya Rais wa China, Xi Jinping kuja Tanzania. “Kwa nini tuone kero kwa Waamerika au kwa nini Wachina wachukiwe kwa ushirikiano wao? Tunashirikiana nao katika nyanja tofauti. Tunafaidika kwa mambo mengi, kwanza tunaangalia misaada ya maendeleo kutoka Marekani, Japan, China, France, Ujerumani na popote pale. Vilevile tunaangalia uwekezaji na masoko ya bidhaa zetu,” anasema. Anaendelea kusisitiza ushirikiano na mataifa ya Asia, Ulaya na Marekani kwa lengo la kukuza uchumi. “Iwe Marekani kaskazini, kusini, Asia na kwingineko, ni ushirikiano tu. Ndiyo maana ukuaji wa uchumi wa Afrika unakua kwa kasi ya asilimia 6.6. ni uchumi unaokuwa kwa kasi ukifuatia bara la Asia.” Ushindani wa Marekani na China Ziara ya Obama imekuja ikiwa ni miezi michache tangu alipokuja Rais wa China, Xi Jingping ambaye naye alisaini mikataba 17 ya miradi ya maendeleo. Marekani yenyewe imewekeza katika miradi ya umeme ambapo kampuni ya Simbion inazalisha megawati 400 mkoani Mtwara na megawatt 100 Ubungo Dar es Salaam, huku kampuni ya Jacobson inazalisha megawati 200 Ubungo. Uwekezaji huo utasaidia kuongeza kiwango cha umeme kwani hadi sasa mahitaji ya umeme ni megawati 1100 na unaozalishwa ni megawati 675 tu, hivyo kupunguza tatizo la umeme linaloikabili asilimia 80 ya Watanzania. Kupitia mradi wa Millennia Challenge Corporation, Marekani imesaidia kutokomeza ugonjwa wa malaria visiwani Zanzibar katika mradi wake uliogharimu dola 698. Vilevile kuna miradi ya ujenzi wa barabara na chuo cha umeme kilichopo mkoani Morogoro. Lakini kila wanachofanya Marekani, China wanafanya kwa nguvu zaidi. China inajenga mradi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam utakaogharimu zaidi ya dola 1 bilioni. Mbali na miradi mingi ya ujenzi nchini, China pia wanajenga daraja la Kigamboni linalogharamiwa na Mfuko wa hifadhi ya jamii (NSSF). Kuna faida au hasara? Wakati mataifa ya Marekani na China yakishindana kuwekeza miradi ya maendeleo nchini, kumekuwa na mtazamo hasi na miradi hiyo huku wengine wakiona kuwa ni mbinu mpya ya mataifa hayo kupora rasilimali. Mhadhiri msaidizi wa Sayansi ya Siasa na utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally anaona ushiriniano wa kasi na mataifa hayo ni kukua kwa itikadi kali ya soko huria duniani. “Zama za Dar es Salaam kuwa kitovu cha mapambano ya ukombozi Afrika zimekwisha eti kwa sababu nchi zote za Afrika ni huru. Wakubwa wa dunia (Marekani, nchi za BRICS na nchi za Umoja wa Ulaya) wanapishana kwenye viwanja vya ndege vya miji mikuu ya nchi za Afrika hasa zile zenye utajiri mkubwa wa raslimali,” anasema Bashiru na kuongeza: “Kinyang’anyiro cha ulimbikizaji wa mitaji na uporaji wa raslimali katika Afrika ni kikali sasa huenda kuliko kile cha enzi za ukoloni. Haishangazi kuona nchi za Afrika Kusini na Tazania zimekuwa na ugeni wa marais wa Marekani na China kwa kipindi kifupi sana.” Bashiru anasema ziara hizi zinafanyika huku vijana wa nchi hizo wakiwa katika mapambano makali na vyombo vya dola vya nchi hizo wakidai mambo mbalimbali yakiwemo mazingira mazuri ya kujikimu na elimu bora isiyo ya kibaguzi. “Hitashangaza ikiwa katika siku za usoni, Dar es Salaam itageuzwa na tabaka kandamizi kuwa Berlin ya Karne ya ishirini na moja. Sote tunaelewa yaliyoisibu dunia na bara la Afrika kutokana na maamuzi ya Berlin ya karne ya kumi na tisa. Afrika iliganywa vipande na kutawaliwa kikoloni kwa karne nzima,” anasema na kuongeza: “Wakati ule Waafrika hawakushiriki katika mikutano ya Berlin ya karne ya kumi na tisa. Waafrika wanaweza kualikwa kama wageni mashuhuri katika mikutano ya Berlin ya karne ya ishirini na moja ikiwa mkakati wa kuiuza Afrika kama bidhaa hautakomeshwa. Hata hivyo, mikutano ya kuligawa bara la Afrika tena itakuwa ya fujo maana wanaotaka kugawana raslimali za Afrika hawataafikiana kirahisi na kizazi cha sasa cha waafrika hakitasalimu amri.” Hata hivyo mawazo ya Bashiru yanapingwa na mwandishi wa habari mwandamizi wa gazeti la Jamhuri, Deodatus Balile alipokuwa akizungumza na Shirika la utangazji la Uingereza (BBC) akisema kuwa ni dhana potofu ya ujamaa na kujitegemea. “Kwa bahati mbaya sana, Watanzania tumelishwa dozi nzuri sana ya ujamaa na kujitegemea, lakini hatukufahamu vizuri maana yake. Kila unayeona ana simu mbili unadhani ni fisadi na kila unayeona ana nyumba mbili basi kakuibia wewe, si kweli,” anasema na kuongeza: “Kwenye uchumi kuna kutegemeana, kwamba huyu anazalisha pamba, huyu ana kiwanda cha kusokota nyuzi na huyu cha kuzalisha suruali, kwa jiyo mnategemeana. Tatizo kuna unyanyapaa, wakisikia Mmarekani wanajua haji hapa kwa wema, wanakumbuka matendo yake Iraqi, Afghanistan, Libya, wanadhani hayo ndiyo yanamleta Tanzania,” anasema Balile. Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba anashauri nchi za Afrika kuwa na mkakati wa pamoja wa kulinda rasilimali zao. “Nchi za Afrika zenye bidhaa ghafi zingekuwa na utaratibu wa pamoja wa kujua namna gani tunaingia kwenye mazunguzo ya kuwa na mahusiano ya kibiashara na wenzetu tuweze kulinda maslahi ya nchi zetu,” anasema Profesa Lipumba. Wananchi wengi walikuwa na sahahuku ya kumwona Obama bila mafanikio. Wengi wameishia kumwona tu kwenye TV akihutunia.

OBAMA TANZANIA

Wananchi wengi walikuwa na sahahuku ya kumwona Obama bila mafanikio. Wengi wameishia kumwona tu kwenye TV akihutunia.