Friday, May 31, 2013

MATOKEO YA KITADO CHA SITA NA CHA NNE..

Matokeo ya kidato cha nne na kidato cha sita yatoka,yameongeza kwa asilima tisa.HONGERA KWA WOTE MLIFANYA VIZURI LAKINI POLENI PIA KWA WALE MLIFANYA VIBAYA kuna msemo unaosema "KIFELI MTIHANI SIO KUFELI MAISHA"bado unanafasi nzuri ya kufanikiwa katika maisha endapo utajituma huku ukimtanguliza MUNGU katika kila kitu unachokifanya sambamba na kutumia rasilimali zilizokuzunguka vizuri.ilikupata matokeo waweza kutembelea website hii www.necta.go.tz

Tuesday, May 28, 2013

"NGWAIR" msanii wa hip hop Tanzania afariki dunia

R.I.P Albet Mangwair •28 May 2013 Kiongozi wa kundi la cowboy mkali wa freestyle ambae alikua akiimba nyimbo za aina HIP HOP amefariki dunia huko nchini South Africa siku ya jumanne na mwili wake umehifadhiwa kwenye hospitali ya st.Hellen kwajili ya mipango ya mazishi.

Monday, May 6, 2013

MIGOGORO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI RUFIJI

Siri mgogoro wakulima, wafugaji Rufiji yabainika Naibu Waziri adaiwa kuchochea Elias Msuya Picha zikionyesha jamii za wafugaji wilayani Rufiji na mifugo yao. Nyingine ni Afisa Ardhi, Mifugo na Mazingira wa wilaya hiyo, Leo Rwegassira. Mgogoro kati ya wakulima na wafugaji wilayani Rufiji unaelezwa kusababishwa na kauli za viongozi wa Serikali huku viongozi wa wilaya hiyo na vijiji wakiwageuza wafugaji hao kuwa kitega uchumi kwa kuwadai rushwa. Mgogoro huo ulianza mara baada ya wafugaji waliokuwa katika bonde la Ihefu mkoani Mbeya kuhamishwa na wilaya ya Rufiji ikafanywa kuwa moja ya maeneo ya kufikia wafugaji hao. Mwezi Mei mwaka 2012 zilizuka vurugu katika kata ya Ikwiriri wilayani humo zilizosababisha watu kujeruhiwa na mali kuharibiwa ikiwa pamoja kuvunjwa kwa nyumba za wafugaji baada ya mkulima mmoja wa kijiji cha Muyuyu kudaiwa kuuawa na wafugaji. Wakizungumzia vurugu hizo katika ziara iliyofanywa na Shirika la kutetea wafugaji wa asili (Pingos Forum) wilayani humo hivi karibuni, baadhi ya wafugaji walimtuhumu Naibu Waziri wa Afya Dk Seif Rashid wakisema kuwa hotuba zake ziliwahamasisha wakulima kuwashambulia. “Vurugu zilianza baada ya baadhi ya wafugaji katika kijiji cha Muyuyu kudaiwa kulisha kwenye shamba la mkulima ambaye baadaye alifariki dunia. Lakini Mbunge alikuwa akihutubia mikutano na kuwaambia wakulima kuwa lazima watuondoe,” alisema Lago Laluka aliyevunjiwa nyumba. Naye Abdallah Nyalando aliyevunjiwa kiwanda cha kusindika maziwa alisisitiza madai hayo: “Ninao ushahidi wa video zikimwonyesha mbunge wetu akiwahamasisha wakulima kuwaondoa wafugaji kwenye maeneo yao,” alisema Nyalando. Hata hivyo Naibu Waziri Dk Seif Rashid amekanusha madai hayo akisema alikuwa akitekeleza uamuzi wa Baraza la Madiwani la wilaya hiyo. “Unajua mtu anaweza kusema lolote, hata hapa tunapozungumza unaweza kuyatafsiri maneno yangu unavyotaka. Nilichokisema mimi ni kuhusu uamuzi wa Baraza la madiwani wa Halmashauri ya Rufiji kwamba bonde hilo litumike kwa ajili ya kilimo siyo mifugo. Lengo ni kulitunza na uharibifu wa mazingira. Siyo Dk Seif kasema ni Halmashauri,” alisema Dk Rashid. Dk Rashid ambaye ni mbunge wa Rufiji amesisitiza kuwa eneo hilo siyo la wafugaji. “Hilo tatizo liko nchi nzima na hata kabla sijawa Mbunge nililifahamu na nilipokwenda Bungeni nilimuuliza Waziri wa Mifugo akanijibu kuwa eneo hilo siyo la wafugaji bali ni la kilimo tu,” alisema. Akizungumzia uamuzi wa Mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza aliyeagiza kuwa wafugaji hao wasiondolewe hadi watakapopatiwa maeneo mengine, alisema kauli hiyo si lolote kama haifuati sheria ya mwaka 1975. “Agizo la mkuu wa mkoa linapaswa kwenda na sheria ya mwaka 1975 inayotaka bonde hilo liwe la kilimo na Waziri alishajibu hivyo,” alisisitiza Dk Rashid. Dk Rashid amedaiwa kutoa kauli za kuwachochea wakulima kuwaondoa wafugaji hao kwa madai ya kuingilia mashamba ya wakulima siku chache kabla ya kutokea vurugu hizo. Baadhi ya wakulima wa Ikwiriri wilayani humo wameilaumu Serikali kwa kutowaelekeza wakulima kwenye maeneo waliyopangiwa. “Serikali ndiyo imewaelekeza wakulima kuja hapa Rufiji na kila siku wanachukua fedha za vibali lakini wameshindwa kuwapeleka kwenye maeneo yao,” alisema Juma Ngwele. Naye Mwajuma Mwinyikambi aliwalaumu wafugaji kwa kulisha mifugo yao kwenye mashamba ya watu. “Tangu wamekuja hao wafugaji hapa amani imepotea kabisa, kwa kweli hatuwataki. Ni kweli tunapata maziwa na nyama kwa urahisi lakini ni wakorofi, wanaharibu mazao yetu kila mara,” alilalamika Mwajuma. Kauli ya mkuu wa mkoa Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza alisema agizo lake lilikuwa ni wakulima kwenda kwenye maeneo waliyopangiwa na siyo vinginevyo. “Agizo langu lilikuwa ni la mpango kazi. Mwaka 2008 wakati Serikali inawahamisha wafugaji kutoka bonde la Ihefu, wilaya ya Rufiji ilikuwa ni moja ya maeneo waliyotakiwa kufikia…Nilichoagiza ni wakulima kwenda kwenye maeneo waliyopangiwa, siyo vinginevyo,” alisema Mahiza na kuongeza: “Wafugaji waliokwenda kwenye maeneo yao waliyopangiwa, tumewaacha, ila wale walio kwenye maeneo yasiyoruhusiwa waondoke.” Serikali haikujiandaa? Akizungumzia kero za wafugaji wilayani humo, Afisa ardhi, maliasili na mazingira, Leo Rwegasira amekiri kwamba Serikali haikuwa imeandaa maeneo ya kuwaweka wafugaji baada ya kuhamishwa kutoka bonde la Ihefu. “Kabla ya kuja wafugaji hawa hapa Rufiji palikuwa shwari, lakini walipokuja mwaka 2007 imekuwa ni vurugu tupu. Awali tuliambiwa kuwa kuna mifugo itakayobaki hapa, mingine itakwenda Lindi na Mtwara hivyo maeneo yaandaliwe. Lakini hadi wanafika hakukuwa na maeneo ya kuwaweka na hakukuwa na fedha za kuainisha maeneo hayo,” alisema Rwegasira. Kutokana na hali hiyo alisema kuwa walitenga vijiji tisa ambavyo waliainisha maeneo ya wafugaji haraka haraka. “Wafugaji wengi walipokuja walifikia kijiji cha Muyuyu kando yam to Rufiji, hata wale waliotakiwa kwenda Lindi na Mtwara wakaishia kando yam to huo,” alisema. Akizungumzia uwezo wa eneo hilo kuchukua mifugo alisema kuna hekta 7874 zenye uwezo wa kuchukua mifugo 39,362 lakini hadi sasa kuna mifugo 109,239. “Hadi sasa tumetenga vijiji 39 ili tuainishe maeneo ya wafugaji na zinatakiwa sh81 milioni na kati ya hizo Halmashauri imetenga sh10 milioni. Ndiyo maana tumewaambia wafugaji nao wachangie sh170, 000 kila mmoja, lakini hawataki, ndiyo maama mgogoro hauishi,” alisema. Akizungumzia kampuni ya Mkiu Poultry farm iliyopewa eneo la uwekezaji badala ya wafugaji wa ng’ombe, Rwegasira alisema huo ulikuwa ni uamuzi wa vijiji hivyo na walipata kibali cha kamishna wa ardhi. Hata hivyo Waziri wa Maendeleo ya mifugo na uvuvi Dk David Mathayo amekanusha kuwa Serikali ilikurupuka kuwahamisha wafugaji hao. Dk Mathayo amekwenda mbali zaidi na kusema kuwa Tume ya matumizi bora ya ardhi inayoshirikisha wizara za Maliasili na Utalii, Mifugo na uvuvi na wizara ya ardhi inaendelea na upimaji wa maeneo ya wafugaji wanaohamishwa. “Kila Halmashauri ina utaratibu wake siwezi kuingilia, lakini kunaTume ya matumizi bora ya ardhi inayohusisha wizara za Maliasili na utalii, Mifugo na Uvuvi na wizara ya Maji inayoainisha maeneo ya wafugaji,” alisema Dk Mathayo na kuongeza: “Tumetenga kiasi cha sh1.2 trilioni kwa ajili ya kazi hiyo iliyoanza miaka mitatu iliyopita. Tumeshapima mikoa 19 kutoa Dar es Salaam, wilaya 66 na vijiji 445. Mwisho wa kazi hii utategemea upatikanaji wa fedha.” Rushwa yatawala Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili wilayani humo umebainisha kuwa Serikali haikuwa imetayarisha eneo maalum la kuwahamishia wafugaji hao hali inayowafanya wasumbuliwe na viongozi wa vijiji wanaowadau fedha ili wawape waeneo ya kulisha mifugo hiyo. Mmoja wa wafugaji hao kutoka kijiji cha Muyuyu, Mbuga Pawa alisema kuwa tangu walipofika wilayani humo wamekuwa wakilipia fedha za usajili kila unapokuja uongozi mpya. “Mara ya kwanza tulipokuja tulilipia vibali vya kukaa vijiji kwa sh30,000, baadaye tukaambiwa siyo halali, tukasajiliwa tena kwa vibali vingine kwa sh80,000 na wengine sasa wanasajiliwa kwa sh100,000. Hadi sasa hatujui hasa ada ya kusajiliwa ili tupewe maeneo ni shilingi ngapi,” alisema Pawa. Naye Joseph Bangi, mfugaji katika kijiji cha Nyamisati anasema mara kwa mara amekuwa akifuatwa na viongozi wa kijiji wakimsumbua na kumdai fedha. “Nilihamia hapa kutoka bonde la Ihefu mwaka 2006 nikalipishwa sh150,000 kama ada ya kufikiriwa na kijiji. Mwaka 2007 nikalipishwa tena sh150,000 na mwaka huu nimelipishwa sh50,000, nimeshatoa sh40,000. Ilimradi kila siku ni kufuatwafuatwa tu, ukilipa kibali hiki kesho unaambiwa siyo halali, unalipa tena,” anasema Bangi. Wafugaji wengine wa jamii ya mang’ati, Saleh Chafuchafu, Masharubu Chafuchafu na Masauda Chafuchafu wanalalamika kufukuzwa katika vijiji vya Kilimani A na B licha ya kuishi tangu mwaka 2006. Mbali na malalamiko ya rushwa, mwezi Aprili mwaka huu, Saleh Chafuchafu amejikuta akilimwa faini ya sh4,080,000 kwa kile kinachodaiwa kuwa mifugo yake iliingilia shamba la mtu. Akizungumzia tuhuma hizo, Afisa mtendaji wa kata ya Ngorongo Uwesu Mbembeni amekiri kuwepo kwa vitendo vya rushwa huku akimtaja aliyekuwa Mwenyekiti wa kijiji cha Ngorongo Magharibi Hassan Mpange kuwa alikusanya kiasi cha sh665,000 kwa wafugaji akidai ni ada ya kuwajadili ili waruhusiwe kuishi na mifugo yao. “Ni kweli kuna mwenyekiti wa zamani wa kijiji cha Ngorongo alichukua sh665,000 za wafugaji 19 akisema ni ada ya kijiji kuwajadili. Lakini fedha hizo hazikufika katika serikali ya kijiji. Mimi nilimwita ofisini kwangu nikamwambia awe tayari kwenda mahakamani,” alisema Mbembeni. Juhudi za kumpata Hassan Mpange kujibu tuhuma hizo hazikufanikiwa kutokana na kukata simu kila anapopigiwa. Akizungumzia eneo walilofikia wafugaji hao ambalo sasa wamefukuzwa na kupewa mwekezaji (Mkiu Poultry Farm) anayelitumia kufugia kuku, Mbembeni alisema: “Ni kweli wafugaji walitangulia katika eneo hilo lakini hawakuwa na vibali halali vya kuishi hapo na mkuu wa wilaya aliafiki kwamba waondolewe.” Amebainisha kuwa mwekezaji huyo alipewa eneo la vijiji vya Ngorongo Magharibi na Mashariki lenye hekta 2026 na kuwaacha wafugaji waliolipia hela zao solemba. Hata hivyo alisema kuwa Mkuu wa mkoa wa Pwani alikataza wafugaji hao kusumbuliwa hadi litakapotafutwa eneo jingine. Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji cha Ngorongo Magharibi Mohamed Mkwega amekiri kuchukua fedha za wafugaji hao akidai ni ada ya uvamizi na posho za kikao. Katika risiti za malipo hayo (nakala tunazo) zilizotolewa Februari 11 mwaka huu, Mwenyekiti huyo alikusanya kiasi cha sh1.8 milioni kutoka kwa wafugaji akidai ni ada ya kikao cha kuwajadili. “Ni kweli tulichukua fedha hizo, ndiyo utaratibu wa kijiji chetu wala siyo utapeli. Fedha hizo zimetumika kama posho za vikao vya kuwajadili kwani kila mjumbe hulipwa sh2000,” alisema Mkwega. Hata hivyo alikiri kuwepo kwa vitendo vya rushwa na kwamba kuan wakati viongozi wa vijiji hutoa hati feki kwa wafugaji. Naye afisa mtendaji wa kijiji hicho, Juma Kilalile alisema tatizo la wafugaji katika vijiji hivyo kuzidiwa na idadi ya mifugo. “Tulifanya sensa ya mifugo tukakuta kuwa kuna zaidi ya ng’ombe 6,000 wakati uwezo wetu ni ng’ombe 130 tu,” alisema. Takukuru Rufiji Akizungumzia malalamiko hayo ya rushwa, Afisa wa Taasisi ya kupamabana na kuzuia rushwa (Takukuru) wilayani Rufiji, Saada Mzimba amekiri kuyapata malalamiko ya rushwa kutoka kwa wafugaji na kwamba tayari kuna kesi mbili baada ya malalamikio hayo. “Ni kweli tunapata malalamiko hayo, kwa mfano kuna wafugaji kutoka kijiji cha Mkongo walifika hapa kulalamika. Huwa tunauliza kama wamepata vibali vya kuishi vijiji hivyo, maana wengine wanavamia tu.,” alisema na kuongeza: “Hadi sasa tuna kesi mbili tumewafungulia viongozi wa vijiji wanaodai rushwa. Vilevile tunawashauri waende kwenye maeneo waliyoandaliwa badala ya kutangatanga.”