Tuesday, February 24, 2015



Tanzania yashutumiwa kwa kunyanyasa wananchi wanaoishi karibu na hifadhi

Elias Msuya



Mwanamke wa Kimasai akiwa na watoto wake baada ya kuchomewa nyumba yake
CHAMA cha kimataifa cha kutetea jamii za watu wanaoishi karibu na hifadhi za Taifa (Indigenous peoples’ and community conserved territories and areas (ICCAs) kimeshutumu hatua ya Serikali ya Tanzania kuwafukuza wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya hifadhi kikisema kuwa ni kinyume na haki za binadamu.

Katika taarifa yake ya Februari 17, ICCA yenye makao yake makuu Geneva Uswisi imeitaja operesheni iliyofanyika katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti ya kuviondoa vijiji vya Ololosokwan na Arash vilivyopo Loliondo wilayani Ngorongoro mkoa wa Arusha kwa kuchoma moto makazi ya wananchi kwa madai ya kuvamia eneo la hifadhi.
Boma la Wamasai likiunga wilayani Ngorongoro

“Ieleweke kwamba, uharibifu huu wa mali umeripotiwa kufanyika nje ya mipaka ya hifadhi kwenye ardhi za vijiji. Ndicho kilichotokea Loliondo na imekuwa chanzo cha migogoro mamlaka za Serikali na wanavijiji ukiwemo mgogoro wa mwaka 2009,” imesema taarifa ya chama hicho.

Mwaka 2013 eneo hilo hilo lilihusishwa katika mgogoro wa kitaifa na kimataifa baada ya serikali ya Tanzania kudaiwa kutaka kuligeuza kuwa pori la akiba na kuwaondioa wananchi wapatao 25,000. Hata hivyo Waziri Nyalandu alikanusha taarifa hizo akisema ni uzushi.

“Mgogoro ulioripotiwa Loliondo ni ukatili ulioshtua katika sera za serikali za hifadhi na vyombo vya sheria na wanajamii,” imesema ICCA.

Chama hicho pia kimelitaja eneo la Ngorongoro lenye zaidi ya watu 60,000 wenye uhaba wa chakula kutokana na vikwazo walivyowekewa na Serikali kwa kuwa eneo hilo ni la urithi wa dunia.

“Maeneo mengine yamekuwa katika mizozo kama hiyo ni pamoja na kijiji cha Kimotorok karibu na hifadhi ya Taifa ya Tarangire, bonde la mto Kilombero na bonde la Usangu lililo karibu na hifadhi ya Taifa ya Ruaha,” ICCA. 

Kauli ya Serikali

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Adelhelm Meru
Akizungumzia operesheni iliyofanyika Loliondo hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Wizaraya Maliasili na Utalii, Dk. Adelhelm Meru alikanusha wananchi kuchomewa nyumba akisema ni mabanda tu yaliyochomwa.

“Hakuna nyumba iliyochomwa pale wala hakuna mtu aliyevunjiwa nyumba. Yale ni mabanda tu, si unajua tena wafugaji wana tabia ya kujenga mabanda na kuhamishia mifugo yao kwenye hifadhi? Halafu wakiachwa wanahamia hapo,” alisema Dk. Meru na kuongeza:

“Tulichofanya ni kuwafukuza na kuyavunja mabanda kwa kutumia kikosi cha Tanapa. Hakuna aliyeumia wala hakuna aliyekufa, ni amani tu.”

Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema hana taarifa ya operesheni hiyo.
             
Vitongoji vya hifadhi ya Saadani

Hivi karibuni chama hicho kiliiandikia barua mbili  Serikali ya Tanzania kikiilaumu kwa kutaka kukihamisha kitongoji cha Uvinje kilichopo katika hifadhi ya Saadani wilaya ya Bagamoyo.

Katika barua hizo mbili ya Agosti 14, 2014 na ya Februari 5, 2015, chama hicho kimepinga hatua ya Serikali kuwahamisha wananchi kwenye kitongoji hicho kwa kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

Barua hizo zimetumwa kwa Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maliasili na Mazingira James Lembeli, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Mkurugenzi wa Shirika Hifadhi za Taifa (Tanapa), Allan Kijazi.
Uvinje ni miongoni mwavitongoji vinane vya kijiji cha Saadani na kilitakiwa kiondolewe tangu mwaka 2005 baada ya hifadhi hiyo kupandishwa daraja kutoka pori la akiba na kuwa hifadhi kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Namba 281 la Septemba 16, 2005.
Hata hivyo wananchi wa kitongoji hicho wanadai kuwa Rais Jakaya Kikwete alifika kijijini hapo kabla ya kugombea urais mwaka 2005 na kuwahakikishia kuwa hawataondolewa.
Akizungumzia suala hilo mwishoni mwa mwaka jana, mhifadhi mkuu wa Saadani, Hassan Malungu alisisitiza kuwa kitongoji hicho kimo ndani ya hifadhi kinyume cha sheria na kwamba mambo ya siasa ndiyo yamechelewesha kukiondoa.
Alisisitiza kuwa sheria za hifadhi za Taifa haziruhusu makazi ya watu ndani yake.
“Kwa ufupi tu ukiangalia GN (Tangazo la Serikali) linaonyesha kuwa eneo lote la kitongoji cha Uvinje liko ndani ya hifadhi. Ni kweli lilikuwa eneo la watu ambao walikuwa watumishi wa pori la akiba tangu lilipoanzishwa mwaka 1968. Waliombwa kuondoka lakini waliendelea kuongezeka,” anasema.
Katika moja ya barua hizo, ICCA imesema:
“Tanzania inayoongoza duniani katika uhifadhi ambapo robo ya eneo lake lote ni hifadhi za taifa na maeneo tengefu, lakini sasa imeuga kuwa neo la migogoro, kati ya Serikali, sekta binafsi na wanajamii wanaozunguka maeneo hayo. Ni wazi kwamba matukio haya yanachafua sifa hiyo,”
“Migogoro hii ina matokeo mabaya kwa uhifadhi wa Taifa na mapato ya nchi, hasa kwa kuwa utalii unaiingizia Tanzania jumla ya Dola za Marekani bilioni mbili kwa mwaka,” inasema ICCA.
ICCA imekumbushia mkutano wa Novemba 2014 uliofanyika Sydney nchini Australia ambao zaidi ya watu 6000 duniani kote ikiwemo Tanzania walihudhuria kwa ajili ya kuweka mikakati na hatua katika uhifadhi kwa muongo unaokuja.
“Tanzania ni mfano hai katika hili. Si chini ya vijiji 1,233 vimekuza hekta 2.366 milioni za miti na misitu na uoto wa asili kama maeneo yanayotunzwa na vijiji. Isitoshe, hekta 5.392 milioni za Taifa na maeneo ya vijiji yamekuwa yakitunzwa na wanavijiji. Asilimia tatu ya nchi yote iko chini ya Jumuiya za hifadhi za wanyamapori (WMA) 38 yaliyotengwa na vijiji 148 kwa ajili ya hifadhi za wanyamapori yakiwa yanatunzwa na watu wapatao 440,000,”
Hata hivyo Katibu Mkuu, Dk. Meru aliyeingia wizarani hapo mwishoni mwa mwaka jana alisema bado hajaziona barua hizo.

“Siwezi kuwa na jibu zuri kwa kuwa sijaziona barua zenyewe. Ila niseme tu kwamba, watu wamekuwa na tabia ya kuvamia maeneo ya Serikali. Ardhi inauzwa bei ghali, hivyo mtu anaona njia rahisi ni kuvamia maeneo ya Serikali yawe ya misitu au hifadhi…” alisema.

Ujangili wa meno ya tembo

ICCA haikuacha kuinyooshea kidole Tanzania kwa tatizo la ujangili wa meno ya tembo ikisema zaidi ya asilimia 50 ya tembo wake wameuawa kwa ujangili.

“Kama hiyo haitoshi, Tanzania imekuwa maarufu kwenye vyombo vya habari vya kimataifa kwa tatizo la ujangili. Karibu asilimia 50 ya tembo wake wamepotelea kwenye janga hilo huku Serikali na sekta binafsi vikihusishwa na mauaji ya wanyama kutokana na athari yake katika utalii,” imesema ICCA.

“Kuwaondoa watu wanaomiliki kihalali maeneo yaliyo karibu na hifadhi zilizo maarufu kimataifa na kuchoma nyumba zao ni kitendo cha aibu,” imesema ICCA.