Serikali yakosa Sh340 bil uchimbaji urani
Dar es Salaam. Tanzania imeanza vibaya
usimamizi wa uwekezaji wa madini ya urani, baada ya kushindwa kesi
mahakamani hivyo kukosa karibu Sh340 bilioni.
Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
ilifungua kesi katika Baraza la Kodi ikiituhumu Kampuni ya JSC
Atomredmetzoloto (ARMZ) ya Urusi, kwamba imekwepa kiasi hicho cha kodi
ambacho ilidai kilipaswa kulipwa kama kodi ya ongezeko la mtaji (Capital
Gain Tax).
TRA walishindwa kesi hiyo mara nne na kwa mara ya
kwanza ilikuwa katika Baraza la Rufaa za Kodi (Tax Revenue Appeals
Board), ambako Kampuni ya ARMZ ilikata rufaa katika kesi namba 26 na 27
za 2011 kupinga malipo ya kiasi cha kodi ilichokuwa ikidaiwa.
Baada ya kushindwa katika hatua hiyo, TRA walikata
rufaa mara ya tatu mbele ya Mahakama ya Rufani za Kodi (The Tax Revenue
Appeals Tribunal), lakini walishindwa hivyo kutoa uhalali wa ARMZ
kutolipa fedha hizo.
TRA katika rufani zake walitaka JSC
Atomredmetzoloto (ARMZ) walipe kodi ya ongezeko la mtaji kwa madai
kwamba kampuni hiyo ya kigeni ilikuwa imenunua hisa kutoka Kampuni ya
Matra Resources Ltd, hivyo ilipaswa kulipa fedha hizo kwa mujibu wa
sheria.
Msingi wa madai ya TRA ni Sheria ya Kodi ya Mapato
ya 2014 kifungu cha 90 (1) kama kilivyofanyiwa marekebisho na Sheria
ya Fedha (Finance Act) ya 2012 ambayo ilipitishwa na Bunge ikielekeza
kampuni zinazouza hisa zake kwa kampuni nyingine, kutozwa asilimia 20 ya
kiasi cha thamani ya hisa, ikiwa ni Kodi ya Ongezeko la Mtaji.
Katika madai hayo, TRA ilitaka ilipwe kiasi cha
Dola za Marekani 196 milioni, sawa na asilimia 20 ya thamani ya hisa
zilizouzwa kwa ARMZ (Dola za Marekani 980 milioni) na Dola za Marekani
9.8 milioni ambazo ni ushuru wa stempu kwa mujibu wa sheria ya ushuru ya
2008. Katika hukumu zake, mahakama ilisema hakukuwa na uhamishaji wa
hisa ndani ya Kampuni za Mantra, kwa sababu Mantra Tanzania ni sehemu ya
kampuni tanzu ya Mantra ya Australia.
Kadhalika mahakama ilisema katika uamuzi wake
kwamba, TRA haina uwezo wa kisheria kudai kodi kutoka ARMZ kwa kuwa
kampuni hiyo haikusajiliwa nchini, bali Urusi ambako inapaswa kulipa
kodi zake.
Kauli za TRA, wizara
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo alipoulizwa kuhusu uamuzi huo unaoikosesha Tanzania mabilioni ya
fedha alisema hana taarifa.
“Sina taarifa hiyo, waulize TRA, pengine
wanafahamu,” alijibu Profesa Muhongo kwa ujumbe mfupi wa maandishi
kupitia simu yake ya kiganjani.
Mkurugenzi wa Elimu na Huduma za Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alisema hana taarifa rasmi kuhusu suala hilo.
No comments:
Post a Comment