Moyo: Nilimwangukia Maalim seif akubali matokeo ya uchaguzi 2010
- Ashangaa Rais Dk. Shein na Rais Kikwete kumtenga
Elias
Msuya aliyekuwa Zanzibar
Hivi karibuni Bunge Maalum la Katiba limekabidhi
rasimu ya Katiba inayopendekezwa kwa rais Jakaya Kikwete na rais wa Zanzibar,
Dk Ali Mohamed Shein.
Hata hivyo rasimu hiyo imepokelewa kwa hisia tofauti
huku makada wa CCM wakiiunga mkono na wapinzani wakiipinga.
Kwa upande wa Zanzibar, siyo wapinzani tu
wanaoipinga, bali hata wana CCM wanaojitaja kuwa na uchungu wa visiwa hivyo.
Akizungumza na mwandishi wetu hivi karibuni mjini
Zanzibar, mwanasiasa mkongwe aliyeshiriki Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12,
1964 Hassan Nassor Moyo anasema Katiba hiyo inapingana na Mapinduzi ya Zanzibar
hivyo haikubaliki. Endelea….
Swali: Katiba inayopendekezwa imepiotishwa na sasa
inapigiwa debe kuelekea kwenye kura ya maoni. Nini nafasi ya Zanzibar katika
Katiba hiyo?
Jibu: Siwezi kujibu swali hilo juu juu tu, ila
nitakupa historia ya muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar. Siku ile ya
Aprili 200, 1964 wakati Mzee Karume alipokuja kwenye Baraza la Mapinduzi la
haraka haraka kwamba tumeshaungana.
Mmoja katika wajumbe wenzetu akiitwa Khamis Abdallah
Ameir aliyekuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi aliyekuwa upande wa Pemba.
Akauliza, mbona Mzee Karume mambo haya ya haraka na jam,bo lenyewe kubwa hili?
Wananchi wenyewe hawapo na wala mwansheria wetu hujamwambia ili atushauri?
Basi Mzee Karume alisema kama hamtaki mimi
nitamrudishia Mwalimu Nyerere makaratasi yake. Sisi tukanyamaza kimya. Kwanza
wakubwa zetu kina Seif Abdallah, Abdou Jumbe ambaye hata hivyo hakuwepo.
Alikuwa amekwenda Pemba, Abdulrahman Babu alikuwa Indonesia wakati huo alikuwa
ni Foregn Minister. Tulikuwepo watu wachache tu.
Sasa ikawa kina Seif
Bakari na Said Natepe kidoogo wakawa wanauliza kwa sauti ya chini, Sasa
Mzee Jee yale mambo yetu tuliyopanga kuyafanya kwa mfano elimu ya bure,
kuchukua ardhi, kufanya afya ya bure, kujenga majengo kwa ajili ya wananchi,
itakuwaje?
Mzee Karume akasema yale tutayafanyia kwenye
Serikali yetu wenyewe. Akasema wenzetu Serikali ya Tanganyika wanaitia ndani ya
Serrikali ya Muungano, ndiyo kauli aliyoitoa.
Tukaona basi, maadamu Serikali yetu itakuwepo na
wenzetu ndani ya muungano , basi ya nini?
Kati ya mwaka 1970 hadi 1971, kumbukumbu yangu haiku
sawa kidogo hapo, kulitokea jam,bo kubwa sana wanangu. Mzee Nyerere aliwapeleka
wanajeshi wa Zanzibar jkwenda Msumbiji kwenye mapambano wakati huop bado
haijapata uhuru. Wakapanda meli ya Serikali ya Zanzibar.
Mzee Karume akapata habari, aliwachukua bila
kushauriana na makamu wake. Akaambiwa, ‘hivi una habari kwamba wanajeshi wako
wanachukuliwa kwenda kupigana vita nchini Msumbiji? Yeye akasema hana habari.
Tena akasema ‘basi irejesheni hiyo meli’, kweli meli ikarejeshwa.
Mwalimu Nyerere akasikia kwamba wale askari
uliowatuma Msumbiji wamerejeshwa. Akauliza, wamerejeshwa na nani?’ akaambiwa
kuwa na Karume. Akaagiza Karume aitwe. Kweli ndege ikaletwa hapa kuchukua
Karume.
Walipokutana,
Mwalimu akamuuliza kama kweli amewarejesha askari wale. Akajibu ndiyo, mimi si
ndiyo msaidizi wako wa kwanza? Wale wanakwenda kupigana vita na ni watoto wa
watu, mimi nitawajibu nini wazazi wao watakapouliza?
Mwalimu akaona kuwa ameteleza kama mtu mzima.
Akakubali kusahuriana.
Baada ya siku nne au tano, Karume akaitisha Baraza
la Mapinduzi. Akatuambia, yale mambo yaliyotokea juzi kama ndiyo mtindo ule
itakuwa hatari. Leo watu wanakwenda vitani bila sisi kuwa na habari, si hatari
hiyo?
Akasema kuna haja ya kufanya mabadiliko ambayo pia
yamo kwenye hati za muungano. Tukataka ‘Foreign Affairs’ tugawane. Mabalozi
wakichaguliwa watano huku, watano kule. Siyo kama leo kuna mabalozi 25 wa Bara
pengine huku watatu tu.
La pili ni ulinzi, rais akitangaza vita akubaliane
na rais wa Zanzibar na akubali. La tatu ni uhamiaji, la nne liwe fedha yaani
kila upande uwe na fedha yake na la tano Polisi, kila mmoja na polisi wake.
Tukakaa kitako tukatengeneza barua rasmi. Sina
hakika kama Aboud Jumbe alitia sahihi, lakini tukapeleka kwa Mwalimu tukitaka
mabadiliko. Alishtuka sana, ikabifi aitishe Baraza la Mapinduzi na Baraza la
Mawaziri, (two governments).
Ikaletwa ndege ya kijeshi tukaingia sote na kwenda
Dar es Salaam. Lakini sisi tulitoka na msimamo kwamba kama Mwalimu Nyerere
atazungumza hovyo hovyo basi ‘no more union’. Ndiyo msimamo wetu.
Serikali ya muungano ikatengeneza waraka rasmi na
kila mmoja wetu alikuwa nao wakati wa kikao. Baada ya mkutano ule Mwalimu
akamuuliza katume, ndiyo mnavyokata hivi iwe? Karume akamjibu, waulize hao
wanaume.
Mwalimu alituuliza mara tatu, ndivyo mnavyotaka?
Sisi tukajibu ndivyo tunavyotaka mabadiliko yafanyike kwenye muungano. 1964
hadi 70, tunataka mabadiliko.
Mwalimu mstaarabu, muungwana, siyo mtu wa barabarani
wa kusukumwasukumwa tu. Akasema kama ndiyo mnavyotaka wakati wake bado haya
mabadiliko. Yule mtu mzima mwenye busara. Tukasema basi makaratasi haya yakusanywe
yakwekwe kwenye kabati hadi wakati mwingine na huo ukawa mwisho wa mkutano.
Tumeondoka huku tumekasirika lakini tukarudi tukiwa
na furaha. Huo ndiyo uungwana, ndiyo uongozi, hapana kudharau mwenzako.
Tunapokuchagua kuwa rais usidhani kwamba hakuna wengine wanaoweza kuwa hivyo.
Swali: Kwa nini hamkuuliza huo wakati utafika lini?
Jibu: Wakati si ndiyo huu?
Swali: Kwa nini usiwe wakati ule mlipokuwa
madarakani?
Jibu: Nimekwambia wakati ndiyo huu, aliyekuwa hai
atasema aliyekufa basi. Tumetengeneza Katiba ya kudumu ya muungano mwaka 1977
na mimi nilikuwa mjumbe wa tume ile ya watu 20, mbona hayo madai hatukuyagusa?
Si jumbe si nani, wote hatukugusa.
Swali: Kwa nini?
Jibu: Ndiyo nakwambia wakati wake bado na mtu
mwerevu hagombani na wakati. Lakini leo Rais Jakaya Kikwete Mungu amempa subra
akaona huu ndiyo wakati wa kuwa na Katiba mpya. Si lazila tupeleke mabadiliko
yale yale lakini wapo vijana wataangalia hili na lile linalofaa.
Swali: Hivi karibuni wakati Rais Jakaya Kikwete
akihutubia wakati wa kupokea Katiba inayopendekezwa, alisema wale ambao
hawakuona mabadiliko katuika katiba hiyo wajue wakati wao bado. Huoni anarudia
yale yake ya Mwalimu Nyrere?
Jibu: Ile ya Mwalimu Nyerere na hii ni tofauti.
Unajua muungano huu umeletwa na Serikali mbili. Kwani wakati ule ASP haikuwepo?
Kwani TANU haikuwepo? Kwa nini Mwalimu Nyerere asiitie kwenye vyama hivyo? Kwa
sababu msingi wa muungano huo ulikuwa ni Serikali, ASP haikushauriwa wala TANU
haikujua.
Tumekwenda hivyo hivyo mpaka tunatengeneza Katiba
mpya ya mwaka 1977,
Mwalimu alibadilisha ile kamati ya watu 20 waliounganisha
vyama vya TANU na ASP kwa kazi nzuri tuliyoifanya. Alizungumza na na Jumbe, kwa
nini tusiifanye kuwa kamati ya kutengeneza Katiba. Hakuna vurugu, hakuna
chochote.
Japokuwa Mwalimu alisemwa kwamba kwa nini
hakutengeza Baraza la Katiba (constitutional assembly) lakini sheria haikusema
hivyo, imesema Baraza la kutengeza Katiba siyo watu fulani na fulani.
Ni kweli sisi ni wanachama wote lakini katika ile
‘spirit’ ya chama. Leo unachukua Baraza la Wawakilishi na Bunge la Muungano
unawapa kazi hiyo? Halafu unawaambia wasifanye kwa misimamo ya vyama! Unataka
kutudanganya sisi? Unatufanya sisi watoto wadogo?
Swali: Asingechukua wale angechukua watu gani?
Jibu: Kuna wau 50 milioni katika nchi hii, aina
Fulani Fulani tunao katika nchi hii. Nenda kijijini huko utapata watu wasomi
wastaarabu, wakulima wazuri utapata tu.
Sasa wewe unakwenda kuchukua Wabunge halafu unasema wasiingine mambo ya siasa?
Maana yake Rais kashindwa kuchukua khata katika wale
201, kachukua kwenye makundi ya vyama. Sasa vyama wanatumia nafasi zao na ndiyo
mvutano wote huu mnaouona.
Lakini kama mnachagua wakulima, siyo hawa wasiojua
kusoma, wapo walihitimu vyuo (graduates), mradi hatuna upungufu wa watu sisi
hadi uchukue tu wa vyama tu.
Hayo ndiyo matatizo yake. Mbona Rais mwenyewe
alileta? Kashindwa kujizuia, maana yeye ndiyo angejizuia. Katuambia kwamba yeye
msimamo wake ni Serikali mbili, ndiyo msimamo wa CCM. Kavuruga nay eye ndiyo
chanzo cha matatizo.
Mbona wakati wa Nyerere tumetengeneza Katiba na
hakuna vurugu? Lakini kwa kufanya hivi sasa tumeanzisha mapambano. Mpaka sasa
CCM msimamo wao ni Serikali mbili na wanawahimiza watu wao waende katika
msimamo huo. Hii siyo Serikali ya chama. Chama kimepewa kuongoza siyo kutawala.
Sisi tumefanya mapinduzi, wenzetu wamemwondosha
mkoloni sasa tuko huru. Chama tawala kinamtawala nani? CCM iko kuongoza nchi,
tule, tulale, tupate dawa na afya. Siyo kutawala.
Kama lengo lilikuwa ni kutawala sisi watu wa ASP
tusingekubali kuungana na TANU, kwa sababu haikuwa dhamira yetu hiyo. Sisi
tumeshajitawala, tumtawala nani tena?
Swali: Kuna dhana au madai kwamba, Zanzibar
hamjatimiziwa madai yenu, kama yale ya mwaka 1970-71. Namaanisha kuwa yale
madai yenu hamkuyasimamia mpaka mwisho.
Jibu: Sasa utayasimamia vipi wakati hizi Serikali
zinageuka kila siku? Ni Serikali za CCM lakini viongozi wanabadilika. Kama sisi
wakati wetu tulileta hayo lakini sote hatuko Serikalini na wengine wameshakufa,
hata waliopo akili zetu hazifanyi kazi. Labda Mzee Moyo tu utamkuta anazungumza
vizuri, lakini mwende Mzee Ramadhani Haji, atasema hili ataliacha na kusema
lile kule… Mwende Hamad Ameir… Aboud Jumbe anasubiri kufariki.
Swali: Lakini wewe bado una nafasi ya kumshauri Rais
wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein?
Jibu: Kakataa kuonana na mimi. Unajua mimi ni
mwenyekiti wa kamati ya maridhiano? Unajua kuwa nchi hii kuna wakati watu
walitaka kuuana? Sasa leo unakuja rais unanikataa? Nitakuonyesha picha zangu
siku ile Dk Shein anatangazwa mshindi
Siku hiyo nilipata habari kuwa Rais mstaafu Amani
Karume ananiita nikaonane na maalim Seif (Seif Sharif). Kaja kijana hapa, Eddy
Riyami saa 10 alfajiri siku ya kutangaza matokeo ya mwaka 2010, wakati niko
nyumba ile kule. Akasema ametumwa na Amani Karume uende ukamwone Maalim Seif. Nikauliza,
kuna nini, nikazungumze naye nini? Akasema hajui.
Nikamuuliza Eddy, jee tumeshashindwa? Aka-smile
(tabasamu). Mimi mtu mzima nikaelewa. Nikasema siondoke mpaka nisali. Nikasali
mpaka saa 11.30, tukaondoka na gari yake mpaka kule.
Kule tukaonana na Maalim Seif na vijana wengi
wamekusanyika pale. Gari tuliiacha msikitini kule. Baadhi ya vijana
wakaniuliza, ‘Moyo unakwenda kupigania Serikali yetu?’ Ndiyo mara ya kwanza
naingia kwenye ofisi ya CUF, Mlandege pale.
Nikawakuta vijana wake mashaababi pale, Duni (Juma),
Machano (Khamis), Jussa (Ismail), Al Haji, vijana wake wale anaowategemea.
Maalim Seif akasema nimepata smu kutoka kwa Amani karume kuwa unakuja kuniona,
maana nilitaka nikakoge. Nikamwambia ni kweli. Nikawatoa baadhi ya vijana nje.
Yeye akabaki na Jussa na mimi na Eddy. Bahati nzuri Jussa ni mwanachama wa
kamati yangu.
Nimemweleza Seif saa 1:30 ananitazama tu hasemi
lolote. Mimi sisemi kwa kubabaisha, siyo mtu wa kubabaisha. Wala siogopi,
sikuumbwa kuogopa mimi. Nimepigania uhuru wan chi hii tangu nikiwa mdogo wa
miaka 22 kupitia vyama vya wafanyakazi.
Kwa hiyo sina hofu ya kuzungumza mambo
ninayoyaamini. Wazungu wamenifunga mimi hapa, nikafukuzwa kazi kwa ajili ya
nchi hii. Kwa hiyo inaniuma sana. Mtu asije akachezea kazi afikiri nitamwacha,
no no no no!
Baada ya kumaliza nikamwambia, ‘aliyonituma ndugu
yako Amani Karume kwamba matangazo yakitangazwa ya uchaguzi wenu wa rais,
uheshimu yale matokeo.
Yale matokeo yatakayotangazwa na Serikali naomba
uyaheshimu. Seif akasema kwa sababu umekuja wewe Moyo, nitakubali. Lakini tume
yetu ya uchaguzi lazima tuifanyie mabadiliko huko tunakokwenda. Ndiyo kauli
aliyoitoa. Hakuongeza chochote.
Nikamwambia Jussa pale apige fatah, akapiga, nikashika
njia kuondoka kwenda Ikulu. Siku ile Amani (Karume) alilala Ikulu, hakulala
kwake, maana mambo hayakuwa madogo, angalau kuna ulinzi.
Tena siku hiyo nilipiga suti ya Kaunda, wakati ule
sina kisukari, nilikuwa shaababi. Aliponiona akasema, Moyo umeshakuja eeh?
Anapiga mluzi maana hata baba yake alikuwa akifurahi hupiga mluzi. Basi naye
amerithi kwa baba yake.
Nikamwambia ‘tayari’, akajibu eeeh tayari? Nikasema
tena tayari. Akasema mimi nimekwambia Moyo umekuja hapa kufanya kazi, umekaa
Tanga kule miaka saba, sasa Mungu kakuleta hapa kufanya kazi.Akampigia siku Seif
pale mbele yangu.
Swali: Kwa maana hiyo unataka kusema kuwa Karume
alikupigia simu ukazungumze na Maalim Seif kwa kuwa Dk. Shein hakushinda
uchaguzi?
Jibu: Ndiyo maana yake, wewe ni mtumzima umeniuliza
swali la kiutu uzim, ndiyo maana yake.
Swali: Je, Dk. Shein naye hakukuita?
Jibu: ndiyo maana nilitaka nikuonyeshe picha.
(Anaonyesha picha akiwa anateta jambo na Dk. Shein huku upande mwingine
akionekana mkewe Dk. Shein, Mwanamwema na nyuma yao ni maafisa wengine wa
Serikali).
Hapa Bwawani (hotel) tumekwenda kusikiliza matokeo
ya urais. Usiku walikuja askari wa Polisi wakasema, mzee unatafutwa uende
Bosnia (kule kwa Maalim Seif, Maisara).
Kumbe kule wameshaambiwa kuwa matangazo
ya urais yasitangazwe mpaka Mzee Moyo awepo. Nikaendea mimi kule Maisara, nikakuta vijana wa
Usalama wa Taifa wakanipokea na magari mawili tukaongozana mpaka Bwawani.
Tumefika na kukaa, huyu mimi, yeye na mkewe.
Unaona hapo kwenye picha tunanong’onezana? Kila
nikiiangalia hii picha namshukuru sana mpiga picha huyu amefanya kazi kubwa.
Alikuwa akiniuliza. Leo nasikia Rais Karume
alikupigia simu asubuhi akasema utazungumza na Maalim Seif. Nikamwambia ni
kweli alinituma na matokeo ya mazungumzo yetu utayasikia hapa. Mimi ni Mngoni,
siogopi kitu. Basi yakatangazwa matokeo pale akawa ameshinda. Akatoa hotuba
pale na wakasema ushindi huu ni wetu sote. Halafu anasema leo hanitambui!
Chaguzi ngapi zimefanywa hapa Zanzibar mimi
nilikwenda? Lakini siku ile Amani alisema lazima Mzee Moyo awepo. Kwa sababu anajua kazi yangu, nchi hii
imetulia kwa sababu ya uongozi wangu.
Hii picha unayoiona ni kamati yetu ya maridhiano
ambayo tulikwenda Ikulu kumtembelea Rais Shein. Hapa bado alikuwa akiitambua.
Uchaguzi umefanyika hakuna mtu hata aliyevunjiaka ukucha.
Nilimwambia hii ndiyo kamati ya maridhiano, je
tuivunje maana iliundwa na marais wengine. Akasema kwa nini muivunje na kazi mmeshafanya?
Basi tukaondoka.
Mara ya pili tukaenda tena kupeleka taarifa ya
kamati yetu. Akasema vizuri nitaisoma. Hajatuita mpaka leo. Mpaka katangaza
hadharani kuwa haitambui kamati yetu… kasema hadharani, mimi mtu mzima siwe
kumsingizia rais wangu.
Basi sisi hatuna haja naye, tunakwenda upande wetu
na yeye upande wake, tutakutana tu.
Swali: Sasa turudi kwenye mchakato wa Katiba,
nilikuuliza awali kama masilahi ya Zanzibar yamezingatiwa, maana hata Rais
Shein alisema hivi karibuni kuwa Wazanzibari walishirikishwa?
Jibu; Mimi nasema hatukushirikishwa. Kuchukua
makundi yale ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba siyo kutushirkkisha. Muungano
huu haukuletwa na vyama bali Serikali, wakakutana viongozi wetu ndiyo
tukaungana.
Mimi naweza kumuuliza Dk. Shein kama alipata nafasi
ya kuketi kitako na viongozi wenzake kujadili jambo hilo? Hawakuketi. Mimi
nafasi yangu nimeonana naye mara tatu nikimwambia, kaa kitako mzungumze na wenzako
ili mwe na msimamo mmoja. Anakujibu, tutaangalia bwana. Kwa hiyo Serikali yetu
haina msimamo kama hili.
Kwa hiyo Serikali yetu inaburuzwa tu. Rais Kikwete
akisema ndiyo naye anashauri tu, lakini hana lake pale.
Muulizeni siku moka kama aliwahi kupeleka ushauri
kwa Kikwete?
Swali: Kama hali yote ndiyo hii, umeonyesha
kutokuridhishwa, nini hatima ya Zanzibar?
Jibu: sisi tunaendelea kupambana hadi tutakapopata
Katiba inayoturidhisha.
Swali: Ni kweli mnapambana lakini iaonyesha wenzako
unaowaacha kama vile hawapambani ipasavyo?
Jibu: Ni sawa, mimi nitaacha rekodi kwamba
nilipambana kwa wakati wangu. Limefanikiwa, ahlan wasahlan, halikufanikiwa ahan
wasahlan. Lazima niseme kwamba hivi ndivyo au sivyo tulivyokubaliana.
Swali: Kwa sasa umezeeka, nadhani umeacha vijana
wanaofuata nyayo zako?
Jibu: Vijana gani? Si ndiyo hao ambao wanaangalia,
jambo hili nilikubali au litaharibu ugali wangu?
Swali: Lakini Mzee, pengine vijana hawa au hata Dk
Shein anaogopa kukutwa na yaliyompata Abdou Jumbe?
Jibu: Sawa, lakini Jumbe alipofanya mambo yale
hakutaka ushauri wa mtu.yale mambo aliyakosea. Miminilikuwa Waziri wa Mambo ya
Ndani mwaka 1978 na nilimshauri Jumbe lakini hakukubali. Nilimwandikia barua na
ipo kwenye faili langu hili na yeye alinijibu.
Swali: Katika huu muungano, unalionaje hili suala la
Serikali ya Tanganyika kuwa ndani ya Serikali ya Muungano?
Jibu: Hili ndilo linaloleta matatizo, kwa sababu
wakati ule ubaya wake hatukuujua, tulisema hewala. Kumbe kulikuwa na siri
alikuwa akiijua Mwalimu Nyerere na ndiyo inatusumbua. Watu wameshikilia hivyo
hivyo, kwani mambo hayabadiliki kama Quran?
Tunasikia kuna kamati za kutatua kero za muungano.
Hazisaidii kwa sababu haipo ndani ya Katiba wala haina madaraka, wanadanganyana
tu.
Swali? Umesema kuwa kwa sasa huwezi kukutana na Rais
Shein, vipi Rais Kikwete, hamwezi kukutana mkashauriana haya?
Jibu: Nikutane naye wa nini? Sawa nikikutana naye
nitamsalimia tu lakini kwa sasa sina haja naye. Kwa sababu hata nikimshauri
hatakubali.
Ngoja nikwambie moja, nchi hii tulikuwepo wazee kama
vile Mzee Mtandika marehemu, Mzee Nyamka, Pancras Ndejembi, Mzee Mkali, Hassan
Moyo, Said Natepe na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tabora. Wazee hawa
tulijikusanya kwa uchungu wa nchi yetu na kwenda kuzungumza na mwalimu Nyerere
miaka ya 1981.
Tulipojikusanya mwalimu alisema tumefanya jambo zuri
sana na akatutia moyo. Ikawa kama kuna jambo tunataka kuzungumza na rais basi
tunakwenda tunazungumza na kushauriana. Alitutumia alipokuwa rais na hata
alipostaafu.
Baada ya Mwalimu Nyerere, akaja Ali Hassan Mwinyi,
tukajitambulisha naye akatupokea. Alipomuuliza Mwalimu akasema watumie wazee
hao watakusaidia. Kuna wakati Mwalimu alitaka kumlipua Mwinyi hadharani
kutokana na lile suala la OIC (Jumuiya ya nchi za Kiislamu). Alitaka kuja
kufanya mkutano pale uwanja wa Jangwani.
Tukaenda Butiama kumwona Mwalimu Nyerere. Akauliza
mbona mmekuja usiku na mimi sina habari. Basi tulikaa nyumbani kwake akawatoa
wajuu zake kwenye chumba chao na kutulaza sisi kwenye vitanda vya ‘double
decker’. Hakutaka kabisa tukalale hotelini, mtu mwungwana sana yule. Mtapata
wapi mtu kama Yule?
Tukafanya safari nyingine kwenda kumhani baada ya
kufiwa na kaka yake, wakati huo akiwa ni kiongozi wa South South. Mama Maria
alitaka kutulaza chumbani kwake lakini tulikataa. Mwalimu Nyerere alikuwa
amekwenda Marekani. Mtapata watu kama wale wapi?
Kwa hiyo tulipita utawala wa Mwinyi, tukaja utawala
wa Mkapa, naye akatutambua vizuri tu. Kutoka huyo akaja Rais Kikwete.
Tulikutana na kijana wake (anamtaja) ambaye ni msiri
wake. Huyo akamwambia Rais Kikwete kuna wazee hawa wamekuwa wkishauriana na
marais mambo mbalimbali.
Naye akakubali. Nikawaambia wenzangu na tukafanya
mawasiliano naye.
Ile safari ya kwanza ya Marekani ambayo Rais Kikwete
liifanya akiwa rais, alimpigia simu kijana wake na kumambia kuhusu sisi na
kwamba akirejea atatuona. Kweli naye alikuja kutujulisha.
Basi aliporudi akatuita Dar es Salaam, mimi, wa
Dodoma, wa Tabora, wa dare s saam na wengine wameshafariki. Tukafikia katika
hoteli moja hapo, ilikua tukutane saa tatu asubuhi. Basi ikawa kazi yetu ni
kuhesabu saa tu, tumekuja kuonana naye saa 2;30 usiku, maana hata kwenda
kukojoa huwezi maana unaogopa ukisikia unaitwa na rais.
Basi tukachukuliwa na kwenda nyumbani kwake usiku
ule. Hata kama alitupikia wali basi tuliula ukiwa na baridi vile vile. Tukajitambulisha
na kueleza malengo yetu na yeye akakubali kuwa ni mazuri.
Tuliondoka pale saa 5 usiku na alitupa Sh1 milioni
kila mmoja, akifikiri kuwa tumefuata pesa pale. Alhamdulillah tunamshukuru
hatuachi kutoa shukrani. Lakini ule ndiyo ulikuwa mwisho wa kuonana.
Tuliwahi kuomba tena kukutana naye, lakini alimtuma
kijana wake aje kutusikiliza akisema kuwa rais ana kazi nyingi. Tukamweleza
mambo yetu.
Safari ya tatu, akaja tena Yule kijana akiwa na
maelezo yale yale. Tukamweleza mambo yetu kisha tukarudi hotelini. Mimi nikawaeleza
wenzangu kuwa, sitakuja tena kwa kuwa rais hataki kuja kutuona. Yale maneno
tuliyomweleza mara ya kwanza hakuyapenda. Akufukuzaye hakwambii toka, utaona tu
matendo yake. Hatujawahi
kurudi tena.
Hayo ndiyo matatizo ya viongozi wetu wa sasa,
hawataki kukaa na kushauriana na wazee kuhusu mambo ya nchi. Pengine kuna wazee
wengine wanaomshauri, siyo lazima tuwe sisi.
No comments:
Post a Comment