Mahakama ya rufani imechakachua demokrasia
Elias Msuya
HUKUMU iliyotolewa hivi karibuni na Mahakama ya Rufani nchini kuhusu kesi ya mgombea binafsi, ina utata mkubwa. kama tulivyozoea kusikia mafuta ya dizeli na petroli yakichakachuliwa na mafuta ya taa, basi mahakama hiyo nayo sasa imechakachua demokrasia.
Katika hukumu hiyo, Mahakama hiyo imesema kuwa sulala la mgombea binafsi siyo la kisiasa bali ni la kisiasa hivyo linapaswa kupelekwa Bungeni ili lijadiliwe na kutolewa uamuzi.
Itakumbukwa kuwa shauri hili lilifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na Mchungaji Mtikila katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma na Mahakama hiyo kupitia kwa Jaji Kahwa Lugakingira, ikaruhusu mgombea binafsi mara baada ya vyama vingi kuanza mwaka 1992. Baada ya Serikali kubwagwa, ilikwenda bungeni na kufanya marekebisho ya sheria na kuvifanya vifungu vilivyotajwa na Mahakama kuwa vinatoa fursa ya kuwapo mgombea binafsi, vikaondolewa na kutamka kuwa mtu anaruhusiwa kugombea kupitia vyama vya siasa. Baada ya marekebisho hayo, Mtikila alifungua tena kesi Mahakama Kuu kwa maelezo kuwa marekebisho hayo yanakiuka haki za binadamu na yako kinyume cha Katiba. Safari hiyo jopo la majaji watatu chini ya Jaji Kiongozi Amir Manento likatamka kuwa vifungu vilivyorekebishwa na Bunge vinakiuka Katiba yenyewe. Majaji hao wakaenda mbali zaidi na kumwagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuandaa mazingira kuanzia hukumu hiyo ilipotolewa hadi uchaguzi wa Oktoba kuwe na sheria inayoruhusu mgombea binafsi. Baada ya hukumu hiyo, Serikali haikuridhika ikakata rufani ambayo sasa ndiyo imetolewa huku hivi karibuni kuwa suala hilo si la kuamuliwa na Mahakama, bali Bunge.
Wasiwasi wangu ni kwamba, kwakuwa suala hili limerudishwa Bungeni, serikali italitumia Bunge kama mhuri kuizika kabisa hoja hii. Kwa kuwa Bunge letu limetawaliwa na wabunge wa CCM, ni wazi kuwa wataipinga tu hoja hiyo na ndiyo utakuwa mwisho wake.
Mimi siyo mwanasheria kitaaluma, lakini nashawishika kuona kwamba mahakama ya rufani imekwepa jukumu lake la kisheria na kuliita kuwa la kisiasa.
Ikumbukwe kwamba, madai ya Mchungaji Mtikila yanatokana na Katiba. Anadai kuwa sheria inayokataza mgombea binafsi inapingana na Katiba ibara ya 21 (1) na (2) . Kwa hiyo kinachotakiwa hapa siyo kubadilisha katiba bali ni kuitafsiri Katiba inayotoa haki ya kila raia kuwa huru kushiriki siasa bila kujiunga na chama au kundi fulani.
Katiba ni sheria na kazi ya mahakama ni kutafsiri sheria, hivyo ilipaswa kuitafsiri sheria hiyo kama ilivyoanya kwenye hukumu za awali.
Suala la mgombea binafsi ni haki ya binadamu, ni hali inayotambuliwa na Katiba. Inashangaza kuona serikali yetu inayosema kuwa inafuata misingi ya haki za binadamu ikikiuka haki hii.
Hata tafiti mbalimbali zilizofanywa hapa nchini zimebaini kuwa, Watanzania wengi wanataka haki ya kuwa na mgombea binafsi.
Mfano ni ripoti ya Mchakato wa kujipima kwakutumia utawala bora (APRM) iliyotoka mwaka huu, imebainisha kuwa Watanzania wengi wanataka haki ya kuwa na mgombea binafsi.
Kwa hiyo kwa kuzingatia utamaduni na siasa za nchi yetu, hili nalo lingepasw kuangaliwa.
Ukweli ni kwamba CCM inaiogopa hoja ya mgombea binafsi kwani inaweza kuisambaratisha kabisa. Usione watu wengi wakati huu wa uchaguzi mkuu wakitangaza nia ya kugombea uongozi kwa tiketi ya CCM. Hawana jinsi, maana ukitaka kufanikiwa kirahisi, sharti ujiunge na CCM.
CCM imejilimbikizia ushindi kiasi kwamba mtu akienda kugombea kwa vyama vya upinzani inambdi awe na moyo wa jiwe.
Wanajua kama sheria ya mgombea binafsi ikipitishwa watu wengi maarufu ndani ya chama hicho watakimbia na kugombea kama wagombea binafsi.
Kuna hoja mbalimbali zinasemwa na wanaopinga sheria ya mgombea binafsi. wapo wanaosema kuwa sheria hiyo ikiruhusiwa, kutatokea machafuko, wengine wanahoji, mgombea binafsi atakuwa akidhibitiwa na nani kinidhamu?
Lakini tukumbuke kwamba sheria hiyo ingepitishwa, basi ingeweka miongozo ya kuwadhibiti wagombea binafsi hata wanaposhinda chaguzi.
Huu ni woga wa bure tu kwa serikali kwasababu, zipo nchi kama Marekani, zimeruhusu wagombea binafsi, lakini hakuna athari yoyote. Kibaya zaidi hata wagombea binafsi wanaposimama kugombea wala hawafahamiki kama wale walioko kwenye vyama vikubwa vya Republican na Democratic achilia mbali vyama vingine.
Tukumbuke pia kwamba vyama vya siasa vimekuwa kikwazo kikubwa cha demokrasia hasa kwakuwa vimekuwa kama kampuni za watu Fulani wanaojiona kuwa wamiliki wa vyama hivyo.
Hata kama mgombea anakubalika kwa wananchi, kama “wenye chama” hawamtaki basi hapiti. Huko ni kuchakachua demokrasia. Demokrasia ni uhuru wa watu kuchagua kiongozi wanayemtaka, siyo kuamuliwa na chama wamchague nani.
Mahakama ambayo ndiyo chombo cha kutoa haki kwa wananchi ilipaswa kusimama kidete kupigania haki hii kama ilivyokuwa imefanya mwanzo.
Lakini kwa kitendo hiki, wananchi wameachwa solemba na hawajui tena kama kuna chombo kingine kitakachotutetea katika kupigania haki zao.
Changamoto nyingine inayojitokeza ni marekebisho ya katiba yetu. Wataalamu wengi na wadau wa sherai wamekuwa wakitoa wito wa kurekebishwa kwa Katiba yetu, lakini serikali imekuwa ikipinga.
Matokeo yake sasa Katiba imekuwa ikijichanganya yenyewe kwa kuwa na vifungu vinavyopingana hivyo kuwa na mvurugano katika utawala na wananchi.
Huku ni kuchakachua demokrasia. Demokrasia ambayo tumeiridhia tunaichanganya na matakwa ya watawala wachache wenye lengo la kutawala milele nchi hii.
Elias Msuya ni mwandishi wa makala wa Gazeti la Mwananchi 0754 897 287

No comments:
Post a Comment