Saturday, October 25, 2014

Moyo: Nilimwangukia Maalim seif akubali matokeo ya uchaguzi 2010
  • Ashangaa Rais Dk. Shein na Rais Kikwete kumtenga
 
Elias Msuya aliyekuwa Zanzibar
 
 
 
Hivi karibuni Bunge Maalum la Katiba limekabidhi rasimu ya Katiba inayopendekezwa kwa rais Jakaya Kikwete na rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.
 
Hata hivyo rasimu hiyo imepokelewa kwa hisia tofauti huku makada wa CCM wakiiunga mkono na wapinzani wakiipinga.
Kwa upande wa Zanzibar, siyo wapinzani tu wanaoipinga, bali hata wana CCM wanaojitaja kuwa na uchungu wa visiwa hivyo.
 
Akizungumza na mwandishi wetu hivi karibuni mjini Zanzibar, mwanasiasa mkongwe aliyeshiriki Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 Hassan Nassor Moyo anasema Katiba hiyo inapingana na Mapinduzi ya Zanzibar hivyo haikubaliki. Endelea….
 
Swali: Katiba inayopendekezwa imepiotishwa na sasa inapigiwa debe kuelekea kwenye kura ya maoni. Nini nafasi ya Zanzibar katika Katiba hiyo?
 
Jibu: Siwezi kujibu swali hilo juu juu tu, ila nitakupa historia ya muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar. Siku ile ya Aprili 200, 1964 wakati Mzee Karume alipokuja kwenye Baraza la Mapinduzi la haraka haraka kwamba tumeshaungana.
Mmoja katika wajumbe wenzetu akiitwa Khamis Abdallah Ameir aliyekuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi aliyekuwa upande wa Pemba. Akauliza, mbona Mzee Karume mambo haya ya haraka na jam,bo lenyewe kubwa hili? Wananchi wenyewe hawapo na wala mwansheria wetu hujamwambia ili atushauri?
 
Basi Mzee Karume alisema kama hamtaki mimi nitamrudishia Mwalimu Nyerere makaratasi yake. Sisi tukanyamaza kimya. Kwanza wakubwa zetu kina Seif Abdallah, Abdou Jumbe ambaye hata hivyo hakuwepo. Alikuwa amekwenda Pemba, Abdulrahman Babu alikuwa Indonesia wakati huo alikuwa ni Foregn Minister. Tulikuwepo watu wachache tu.
 
Sasa ikawa kina Seif  Bakari na Said Natepe kidoogo wakawa wanauliza kwa sauti ya chini, Sasa Mzee Jee yale mambo yetu tuliyopanga kuyafanya kwa mfano elimu ya bure, kuchukua ardhi, kufanya afya ya bure, kujenga majengo kwa ajili ya wananchi, itakuwaje?
 
Mzee Karume akasema yale tutayafanyia kwenye Serikali yetu wenyewe. Akasema wenzetu Serikali ya Tanganyika wanaitia ndani ya Serrikali ya Muungano, ndiyo kauli aliyoitoa.
 
Tukaona basi, maadamu Serikali yetu itakuwepo na wenzetu ndani ya muungano , basi ya nini?
 
Kati ya mwaka 1970 hadi 1971, kumbukumbu yangu haiku sawa kidogo hapo, kulitokea jam,bo kubwa sana wanangu. Mzee Nyerere aliwapeleka wanajeshi wa Zanzibar jkwenda Msumbiji kwenye mapambano wakati huop bado haijapata uhuru. Wakapanda meli ya Serikali ya Zanzibar.
 
 
Mzee Karume akapata habari, aliwachukua bila kushauriana na makamu wake. Akaambiwa, ‘hivi una habari kwamba wanajeshi wako wanachukuliwa kwenda kupigana vita nchini Msumbiji? Yeye akasema hana habari. Tena akasema ‘basi irejesheni hiyo meli’, kweli meli ikarejeshwa.
 
Mwalimu Nyerere akasikia kwamba wale askari uliowatuma Msumbiji wamerejeshwa. Akauliza, wamerejeshwa na nani?’ akaambiwa kuwa na Karume. Akaagiza Karume aitwe. Kweli ndege ikaletwa hapa kuchukua Karume.
 Walipokutana, Mwalimu akamuuliza kama kweli amewarejesha askari wale. Akajibu ndiyo, mimi si ndiyo msaidizi wako wa kwanza? Wale wanakwenda kupigana vita na ni watoto wa watu, mimi nitawajibu nini wazazi wao watakapouliza?
 
Mwalimu akaona kuwa ameteleza kama mtu mzima. Akakubali kusahuriana.
Baada ya siku nne au tano, Karume akaitisha Baraza la Mapinduzi. Akatuambia, yale mambo yaliyotokea juzi kama ndiyo mtindo ule itakuwa hatari. Leo watu wanakwenda vitani bila sisi kuwa na habari, si hatari hiyo?
 
Akasema kuna haja ya kufanya mabadiliko ambayo pia yamo kwenye hati za muungano. Tukataka ‘Foreign Affairs’ tugawane. Mabalozi wakichaguliwa watano huku, watano kule. Siyo kama leo kuna mabalozi 25 wa Bara pengine huku watatu tu.
La pili ni ulinzi, rais akitangaza vita akubaliane na rais wa Zanzibar na akubali. La tatu ni uhamiaji, la nne liwe fedha yaani kila upande uwe na fedha yake na la tano Polisi, kila mmoja na polisi wake.
 
Tukakaa kitako tukatengeneza barua rasmi. Sina hakika kama Aboud Jumbe alitia sahihi, lakini tukapeleka kwa Mwalimu tukitaka mabadiliko. Alishtuka sana, ikabifi aitishe Baraza la Mapinduzi na Baraza la Mawaziri, (two governments).
Ikaletwa ndege ya kijeshi tukaingia sote na kwenda Dar es Salaam. Lakini sisi tulitoka na msimamo kwamba kama Mwalimu Nyerere atazungumza hovyo hovyo basi ‘no more union’. Ndiyo msimamo wetu.
Serikali ya muungano ikatengeneza waraka rasmi na kila mmoja wetu alikuwa nao wakati wa kikao. Baada ya mkutano ule Mwalimu akamuuliza katume, ndiyo mnavyokata hivi iwe? Karume akamjibu, waulize hao wanaume.
 
Mwalimu alituuliza mara tatu, ndivyo mnavyotaka? Sisi tukajibu ndivyo tunavyotaka mabadiliko yafanyike kwenye muungano. 1964 hadi 70, tunataka mabadiliko.
Mwalimu mstaarabu, muungwana, siyo mtu wa barabarani wa kusukumwasukumwa tu. Akasema kama ndiyo mnavyotaka wakati wake bado haya mabadiliko. Yule mtu mzima mwenye busara. Tukasema basi makaratasi haya yakusanywe yakwekwe kwenye kabati hadi wakati mwingine na huo ukawa mwisho wa mkutano.
Tumeondoka huku tumekasirika lakini tukarudi tukiwa na furaha. Huo ndiyo uungwana, ndiyo uongozi, hapana kudharau mwenzako. Tunapokuchagua kuwa rais usidhani kwamba hakuna wengine wanaoweza kuwa hivyo. 
 
 
Swali: Kwa nini hamkuuliza huo wakati utafika lini?
 
Jibu: Wakati si ndiyo huu?
 
Swali: Kwa nini usiwe wakati ule mlipokuwa madarakani?
 
Jibu: Nimekwambia wakati ndiyo huu, aliyekuwa hai atasema aliyekufa basi. Tumetengeneza Katiba ya kudumu ya muungano mwaka 1977 na mimi nilikuwa mjumbe wa tume ile ya watu 20, mbona hayo madai hatukuyagusa? Si jumbe si nani, wote hatukugusa.
 
Swali: Kwa nini?
 
Jibu: Ndiyo nakwambia wakati wake bado na mtu mwerevu hagombani na wakati. Lakini leo Rais Jakaya Kikwete Mungu amempa subra akaona huu ndiyo wakati wa kuwa na Katiba mpya. Si lazila tupeleke mabadiliko yale yale lakini wapo vijana wataangalia hili na lile linalofaa.
 
Swali: Hivi karibuni wakati Rais Jakaya Kikwete akihutubia wakati wa kupokea Katiba inayopendekezwa, alisema wale ambao hawakuona mabadiliko katuika katiba hiyo wajue wakati wao bado. Huoni anarudia yale yake ya Mwalimu Nyrere?
 
Jibu: Ile ya Mwalimu Nyerere na hii ni tofauti. Unajua muungano huu umeletwa na Serikali mbili. Kwani wakati ule ASP haikuwepo? Kwani TANU haikuwepo? Kwa nini Mwalimu Nyerere asiitie kwenye vyama hivyo? Kwa sababu msingi wa muungano huo ulikuwa ni Serikali, ASP haikushauriwa wala TANU haikujua.
Tumekwenda hivyo hivyo mpaka tunatengeneza Katiba mpya ya mwaka 1977, 
 
Mwalimu alibadilisha ile kamati ya watu 20 waliounganisha vyama vya TANU na ASP kwa kazi nzuri tuliyoifanya. Alizungumza na na Jumbe, kwa nini tusiifanye kuwa kamati ya kutengeneza Katiba. Hakuna vurugu, hakuna chochote.
Japokuwa Mwalimu alisemwa kwamba kwa nini hakutengeza Baraza la Katiba (constitutional assembly) lakini sheria haikusema hivyo, imesema Baraza la kutengeza Katiba siyo watu fulani na fulani.
 
Ni kweli sisi ni wanachama wote lakini katika ile ‘spirit’ ya chama. Leo unachukua Baraza la Wawakilishi na Bunge la Muungano unawapa kazi hiyo? Halafu unawaambia wasifanye kwa misimamo ya vyama! Unataka kutudanganya sisi? Unatufanya sisi watoto wadogo?
 
Swali: Asingechukua wale angechukua watu gani?
 
Jibu: Kuna wau 50 milioni katika nchi hii, aina Fulani Fulani tunao katika nchi hii. Nenda kijijini huko utapata watu wasomi wastaarabu, wakulima wazuri  utapata tu. Sasa wewe unakwenda kuchukua Wabunge halafu unasema wasiingine mambo ya siasa?
 
Maana yake Rais kashindwa kuchukua khata katika wale 201, kachukua kwenye makundi ya vyama. Sasa vyama wanatumia nafasi zao na ndiyo mvutano wote huu mnaouona.
 
Lakini kama mnachagua wakulima, siyo hawa wasiojua kusoma, wapo walihitimu vyuo (graduates), mradi hatuna upungufu wa watu sisi hadi uchukue tu wa vyama tu.
Hayo ndiyo matatizo yake. Mbona Rais mwenyewe alileta? Kashindwa kujizuia, maana yeye ndiyo angejizuia. Katuambia kwamba yeye msimamo wake ni Serikali mbili, ndiyo msimamo wa CCM. Kavuruga nay eye ndiyo chanzo cha matatizo.
 
Mbona wakati wa Nyerere tumetengeneza Katiba na hakuna vurugu? Lakini kwa kufanya hivi sasa tumeanzisha mapambano. Mpaka sasa CCM msimamo wao ni Serikali mbili na wanawahimiza watu wao waende katika msimamo huo. Hii siyo Serikali ya chama. Chama kimepewa kuongoza siyo kutawala.
 
Sisi tumefanya mapinduzi, wenzetu wamemwondosha mkoloni sasa tuko huru. Chama tawala kinamtawala nani? CCM iko kuongoza nchi, tule, tulale, tupate dawa na afya. Siyo kutawala.
 
Kama lengo lilikuwa ni kutawala sisi watu wa ASP tusingekubali kuungana na TANU, kwa sababu haikuwa dhamira yetu hiyo. Sisi tumeshajitawala, tumtawala nani tena?
 
Swali: Kuna dhana au madai kwamba, Zanzibar hamjatimiziwa madai yenu, kama yale ya mwaka 1970-71. Namaanisha kuwa yale madai yenu hamkuyasimamia mpaka mwisho.
 
Jibu: Sasa utayasimamia vipi wakati hizi Serikali zinageuka kila siku? Ni Serikali za CCM lakini viongozi wanabadilika. Kama sisi wakati wetu tulileta hayo lakini sote hatuko Serikalini na wengine wameshakufa, hata waliopo akili zetu hazifanyi kazi. Labda Mzee Moyo tu utamkuta anazungumza vizuri, lakini mwende Mzee Ramadhani Haji, atasema hili ataliacha na kusema lile kule… Mwende Hamad Ameir… Aboud Jumbe anasubiri kufariki. 
 
 
Swali: Lakini wewe bado una nafasi ya kumshauri Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein?
Jibu: Kakataa kuonana na mimi. Unajua mimi ni mwenyekiti wa kamati ya maridhiano? Unajua kuwa nchi hii kuna wakati watu walitaka kuuana? Sasa leo unakuja rais unanikataa? Nitakuonyesha picha zangu siku ile Dk Shein anatangazwa mshindi
 
Siku hiyo nilipata habari kuwa Rais mstaafu Amani Karume ananiita nikaonane na maalim Seif (Seif Sharif). Kaja kijana hapa, Eddy Riyami saa 10 alfajiri siku ya kutangaza matokeo ya mwaka 2010, wakati niko nyumba ile kule. Akasema ametumwa na Amani Karume uende ukamwone Maalim Seif. Nikauliza, kuna nini, nikazungumze naye nini? Akasema hajui.
 
Nikamuuliza Eddy, jee tumeshashindwa? Aka-smile (tabasamu). Mimi mtu mzima nikaelewa. Nikasema siondoke mpaka nisali. Nikasali mpaka saa 11.30, tukaondoka na gari yake mpaka kule.
 
Kule tukaonana na Maalim Seif na vijana wengi wamekusanyika pale. Gari tuliiacha msikitini kule. Baadhi ya vijana wakaniuliza, ‘Moyo unakwenda kupigania Serikali yetu?’ Ndiyo mara ya kwanza naingia kwenye ofisi ya CUF, Mlandege pale.
 
Nikawakuta vijana wake mashaababi pale, Duni (Juma), Machano (Khamis), Jussa (Ismail), Al Haji, vijana wake wale anaowategemea. Maalim Seif akasema nimepata smu kutoka kwa Amani karume kuwa unakuja kuniona, maana nilitaka nikakoge. Nikamwambia ni kweli. Nikawatoa baadhi ya vijana nje. Yeye akabaki na Jussa na mimi na Eddy. Bahati nzuri Jussa ni mwanachama wa kamati yangu.
Nimemweleza Seif saa 1:30 ananitazama tu hasemi lolote. Mimi sisemi kwa kubabaisha, siyo mtu wa kubabaisha. Wala siogopi, sikuumbwa kuogopa mimi. Nimepigania uhuru wan chi hii tangu nikiwa mdogo wa miaka 22 kupitia vyama vya wafanyakazi.
Kwa hiyo sina hofu ya kuzungumza mambo ninayoyaamini. Wazungu wamenifunga mimi hapa, nikafukuzwa kazi kwa ajili ya nchi hii. Kwa hiyo inaniuma sana. Mtu asije akachezea kazi afikiri nitamwacha, no no no no!
 
Baada ya kumaliza nikamwambia, ‘aliyonituma ndugu yako Amani Karume kwamba matangazo yakitangazwa ya uchaguzi wenu wa rais, uheshimu yale matokeo.
Yale matokeo yatakayotangazwa na Serikali naomba uyaheshimu. Seif akasema kwa sababu umekuja wewe Moyo, nitakubali. Lakini tume yetu ya uchaguzi lazima tuifanyie mabadiliko huko tunakokwenda. Ndiyo kauli aliyoitoa. Hakuongeza chochote.
Nikamwambia Jussa pale apige fatah, akapiga, nikashika njia kuondoka kwenda Ikulu. Siku ile Amani (Karume) alilala Ikulu, hakulala kwake, maana mambo hayakuwa madogo, angalau kuna ulinzi.
 
Tena siku hiyo nilipiga suti ya Kaunda, wakati ule sina kisukari, nilikuwa shaababi. Aliponiona akasema, Moyo umeshakuja eeh? Anapiga mluzi maana hata baba yake alikuwa akifurahi hupiga mluzi. Basi naye amerithi kwa baba yake.
Nikamwambia ‘tayari’, akajibu eeeh tayari? Nikasema tena tayari. Akasema mimi nimekwambia Moyo umekuja hapa kufanya kazi, umekaa Tanga kule miaka saba, sasa Mungu kakuleta hapa kufanya kazi.Akampigia siku Seif pale mbele yangu.
 
Swali: Kwa maana hiyo unataka kusema kuwa Karume alikupigia simu ukazungumze na Maalim Seif kwa kuwa Dk. Shein hakushinda uchaguzi?
 
Jibu: Ndiyo maana yake, wewe ni mtumzima umeniuliza swali la kiutu uzim, ndiyo maana yake.
 
Swali: Je, Dk. Shein naye hakukuita?
 
Jibu: ndiyo maana nilitaka nikuonyeshe picha. (Anaonyesha picha akiwa anateta jambo na Dk. Shein huku upande mwingine akionekana mkewe Dk. Shein, Mwanamwema na nyuma yao ni maafisa wengine wa Serikali).
Hapa Bwawani (hotel) tumekwenda kusikiliza matokeo ya urais. Usiku walikuja askari wa Polisi wakasema, mzee unatafutwa uende Bosnia (kule kwa Maalim Seif, Maisara). 
 
Kumbe kule wameshaambiwa kuwa matangazo ya urais yasitangazwe mpaka Mzee Moyo awepo. Nikaendea mimi kule Maisara, nikakuta vijana wa Usalama wa Taifa wakanipokea na magari mawili tukaongozana mpaka Bwawani. Tumefika na kukaa, huyu mimi, yeye na mkewe.
 
Unaona hapo kwenye picha tunanong’onezana? Kila nikiiangalia hii picha namshukuru sana mpiga picha huyu amefanya kazi kubwa.
Alikuwa akiniuliza. Leo nasikia Rais Karume alikupigia simu asubuhi akasema utazungumza na Maalim Seif. Nikamwambia ni kweli alinituma na matokeo ya mazungumzo yetu utayasikia hapa. Mimi ni Mngoni, siogopi kitu. Basi yakatangazwa matokeo pale akawa ameshinda. Akatoa hotuba pale na wakasema ushindi huu ni wetu sote. Halafu anasema leo hanitambui!
Chaguzi ngapi zimefanywa hapa Zanzibar mimi nilikwenda? Lakini siku ile Amani alisema lazima Mzee Moyo  awepo. Kwa sababu anajua kazi yangu, nchi hii imetulia kwa sababu ya uongozi wangu.
 
Hii picha unayoiona ni kamati yetu ya maridhiano ambayo tulikwenda Ikulu kumtembelea Rais Shein. Hapa bado alikuwa akiitambua. Uchaguzi umefanyika hakuna mtu hata aliyevunjiaka ukucha.
 
Nilimwambia hii ndiyo kamati ya maridhiano, je tuivunje maana iliundwa na marais wengine. Akasema kwa nini muivunje na kazi mmeshafanya? Basi tukaondoka.
Mara ya pili tukaenda tena kupeleka taarifa ya kamati yetu. Akasema vizuri nitaisoma. Hajatuita mpaka leo. Mpaka katangaza hadharani kuwa haitambui kamati yetu… kasema hadharani, mimi mtu mzima siwe kumsingizia rais wangu.
Basi sisi hatuna haja naye, tunakwenda upande wetu na yeye upande wake, tutakutana tu.
 
Swali: Sasa turudi kwenye mchakato wa Katiba, nilikuuliza awali kama masilahi ya Zanzibar yamezingatiwa, maana hata Rais Shein alisema hivi karibuni kuwa Wazanzibari walishirikishwa?
 
Jibu; Mimi nasema hatukushirikishwa. Kuchukua makundi yale ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba siyo kutushirkkisha. Muungano huu haukuletwa na vyama bali Serikali, wakakutana viongozi wetu ndiyo tukaungana.
Mimi naweza kumuuliza Dk. Shein kama alipata nafasi ya kuketi kitako na viongozi wenzake kujadili jambo hilo? Hawakuketi. Mimi nafasi yangu nimeonana naye mara tatu nikimwambia, kaa kitako mzungumze na wenzako ili mwe na msimamo mmoja. Anakujibu, tutaangalia bwana. Kwa hiyo Serikali yetu haina msimamo kama hili.
Kwa hiyo Serikali yetu inaburuzwa tu. Rais Kikwete akisema ndiyo naye anashauri tu, lakini hana lake pale.
Muulizeni siku moka kama aliwahi kupeleka ushauri kwa Kikwete?
 
Swali: Kama hali yote ndiyo hii, umeonyesha kutokuridhishwa, nini hatima ya Zanzibar?
 
Jibu: sisi tunaendelea kupambana hadi tutakapopata Katiba  inayoturidhisha.
 
Swali: Ni kweli mnapambana lakini iaonyesha wenzako unaowaacha kama vile hawapambani ipasavyo?
Jibu: Ni sawa, mimi nitaacha rekodi kwamba nilipambana kwa wakati wangu. Limefanikiwa, ahlan wasahlan, halikufanikiwa ahan wasahlan. Lazima niseme kwamba hivi ndivyo au sivyo tulivyokubaliana.
 
Swali: Kwa sasa umezeeka, nadhani umeacha vijana wanaofuata nyayo zako?
 
Jibu: Vijana gani? Si ndiyo hao ambao wanaangalia, jambo hili nilikubali au litaharibu ugali wangu?
 
Swali: Lakini Mzee, pengine vijana hawa au hata Dk Shein anaogopa kukutwa na yaliyompata Abdou Jumbe?
Jibu: Sawa, lakini Jumbe alipofanya mambo yale hakutaka ushauri wa mtu.yale mambo aliyakosea. Miminilikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani mwaka 1978 na nilimshauri Jumbe lakini hakukubali. Nilimwandikia barua na ipo kwenye faili langu hili na yeye alinijibu. 
 
 
Swali: Katika huu muungano, unalionaje hili suala la Serikali ya Tanganyika kuwa ndani ya Serikali ya Muungano?
 
Jibu: Hili ndilo linaloleta matatizo, kwa sababu wakati ule ubaya wake hatukuujua, tulisema hewala. Kumbe kulikuwa na siri alikuwa akiijua Mwalimu Nyerere na ndiyo inatusumbua. Watu wameshikilia hivyo hivyo, kwani mambo hayabadiliki kama Quran?
Tunasikia kuna kamati za kutatua kero za muungano. Hazisaidii kwa sababu haipo ndani ya Katiba wala haina madaraka, wanadanganyana tu.
 
Swali? Umesema kuwa kwa sasa huwezi kukutana na Rais Shein, vipi Rais Kikwete, hamwezi kukutana mkashauriana haya?
 
Jibu: Nikutane naye wa nini? Sawa nikikutana naye nitamsalimia tu lakini kwa sasa sina haja naye. Kwa sababu hata nikimshauri hatakubali.
Ngoja nikwambie moja, nchi hii tulikuwepo wazee kama vile Mzee Mtandika marehemu, Mzee Nyamka, Pancras Ndejembi, Mzee Mkali, Hassan Moyo, Said Natepe na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tabora. Wazee hawa tulijikusanya kwa uchungu wa nchi yetu na kwenda kuzungumza na mwalimu Nyerere miaka ya 1981.
 
Tulipojikusanya mwalimu alisema tumefanya jambo zuri sana na akatutia moyo. Ikawa kama kuna jambo tunataka kuzungumza na rais basi tunakwenda tunazungumza na kushauriana. Alitutumia alipokuwa rais na hata alipostaafu.
 
Baada ya Mwalimu Nyerere, akaja Ali Hassan Mwinyi, tukajitambulisha naye akatupokea. Alipomuuliza Mwalimu akasema watumie wazee hao watakusaidia. Kuna wakati Mwalimu alitaka kumlipua Mwinyi hadharani kutokana na lile suala la OIC (Jumuiya ya nchi za Kiislamu). Alitaka kuja kufanya mkutano pale uwanja wa Jangwani.
 
Tukaenda Butiama kumwona Mwalimu Nyerere. Akauliza mbona mmekuja usiku na mimi sina habari. Basi tulikaa nyumbani kwake akawatoa wajuu zake kwenye chumba chao na kutulaza sisi kwenye vitanda vya ‘double decker’. Hakutaka kabisa tukalale hotelini, mtu mwungwana sana yule. Mtapata wapi mtu kama Yule?
 
Tukafanya safari nyingine kwenda kumhani baada ya kufiwa na kaka yake, wakati huo akiwa ni kiongozi wa South South. Mama Maria alitaka kutulaza chumbani kwake lakini tulikataa. Mwalimu Nyerere alikuwa amekwenda Marekani. Mtapata watu kama wale wapi?
 
Kwa hiyo tulipita utawala wa Mwinyi, tukaja utawala wa Mkapa, naye akatutambua vizuri tu. Kutoka huyo akaja Rais Kikwete.
Tulikutana na kijana wake (anamtaja) ambaye ni msiri wake. Huyo akamwambia Rais Kikwete kuna wazee hawa wamekuwa wkishauriana na marais mambo mbalimbali. 
 
Naye akakubali. Nikawaambia wenzangu na tukafanya mawasiliano naye.
Ile safari ya kwanza ya Marekani ambayo Rais Kikwete liifanya akiwa rais, alimpigia simu kijana wake na kumambia kuhusu sisi na kwamba akirejea atatuona. Kweli naye alikuja kutujulisha.
 
Basi aliporudi akatuita Dar es Salaam, mimi, wa Dodoma, wa Tabora, wa dare s saam na wengine wameshafariki. Tukafikia katika hoteli moja hapo, ilikua tukutane saa tatu asubuhi. Basi ikawa kazi yetu ni kuhesabu saa tu, tumekuja kuonana naye saa 2;30 usiku, maana hata kwenda kukojoa huwezi maana unaogopa ukisikia unaitwa na rais.
Basi tukachukuliwa na kwenda nyumbani kwake usiku ule. Hata kama alitupikia wali basi tuliula ukiwa na baridi vile vile. Tukajitambulisha na kueleza malengo yetu na yeye akakubali kuwa ni mazuri.
 
Tuliondoka pale saa 5 usiku na alitupa Sh1 milioni kila mmoja, akifikiri kuwa tumefuata pesa pale. Alhamdulillah tunamshukuru hatuachi kutoa shukrani. Lakini ule ndiyo ulikuwa mwisho wa kuonana. 
 
 
Tuliwahi kuomba tena kukutana naye, lakini alimtuma kijana wake aje kutusikiliza akisema kuwa rais ana kazi nyingi. Tukamweleza mambo yetu.
 
Safari ya tatu, akaja tena Yule kijana akiwa na maelezo yale yale. Tukamweleza mambo yetu kisha tukarudi hotelini. Mimi nikawaeleza wenzangu kuwa, sitakuja tena kwa kuwa rais hataki kuja kutuona. Yale maneno tuliyomweleza mara ya kwanza hakuyapenda. Akufukuzaye hakwambii toka, utaona tu matendo yake. Hatujawahi 
 kurudi tena.
 
Hayo ndiyo matatizo ya viongozi wetu wa sasa, hawataki kukaa na kushauriana na wazee kuhusu mambo ya nchi. Pengine kuna wazee wengine wanaomshauri, siyo lazima tuwe sisi.