Friday, September 23, 2011
MV SPICE ISLANDER, NANI ALAUMIWE?
Meli ilivyozama
Mbunge wa Ziwani Ahmed Ngwali akiorodhesha majina ya walioathiriwa
Makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar Seif Sharif Hamad na maafisa wengine wa serikali hiyo wakiwahami waliofiwa
Elias Msuya
TUKIO la kuzama kwa meli ya Mv Spice Islander lililotokea hivi karibuni katika eneo la Nungwi na kusababisha vifo, majeruhi na watu wengi kupotea, limefufua hisi nyingi za mionmgoni mwa Wazanzibar.
Licha ya serikali ya Zanzibar kutangaza kufanya uchunguzi, maswali mengi yameanza kujitokeza kuhusu utendaji wa serikali hiyo ambayo kwasasa inahusisha vyama vya CUF mna CCM.
Wakazi wa kisiwa cha Pemba ambao kimsingi ndiyo wamepata msiba mkubwa kutokana na ajali hiyo, wameibuka na hisia za kutengwa licha ya chama cha Wananchi (CUF) ambacho ngome yake iko kisiwani humo kuwa serikalini.
Katika msiba huo, wananchi wengi wamepoteza dugu na jamaa zao. Lakini kwa Rashid Abdallah Rashid anayeishi Shehia ya Jadida wilayani Wete msiba huo kwake umekuja mara mbili, kwani ndugu zake waliokuwa wakija kuhani msiba uliotokea kwake, waliishia kufa kwenye ajali hiyo.
Rashid ambaye anasema bado wako kwenye jitihada za kuwatafuta ndugu zao, anasema kuwa kati ya ndugu 30 waliosafiri siku hiyo, hadi sasa wamepata maiti nne na watu walio hai watatu.
“Siku ya Ijumaa tulipata msiba wa dada ambaye alianguka kwenye pikipiki na kugongwa na gari. Kwakuwa kichwa kilisagika vibaya, tulimzika siku hiyo hiyo. Tukawajulisha ndugu zetu wa Unguja na kwingineko waje. Ndiyo hao wameishia kwenye ajali ya Mv Spice Islander” anasema Rashid.
Rashid anaelekeza lawama kwa serikali ya Zanzibar, akisema kuwa imezembea kwakuwa wengi wa abiria waliokuwamo walitoka Pemba.
“Japo ajali hii ilipangwa na Mwenyezi Mungu, kuna uzembe mkubwa uliofanywa na serikali. Tukio hilo lilianzia bandarini, wahusika waliona, taarifa za kuzama kwa meli zilianza kupatikana tangu saa nane kasorobo, serikali haikuchukua hatua yoyote, hadi saa mbili asubuhi zilipoletwa helkopita” anasena Rashid na kuongeza,
“Kama wangekuwa watu wa Bara, Kikwete asingekubali, wangekuwa Waunguja, hatua zingechukuliwa mapema. Lakini kwakuwa sisi ni Wapemba, hatukubaliki siku zote”.
Anaendelea kulalamika kuwa ubovu wa vyombo vya usafiri na usafirishaji vinavyofanya safari zake kisiwani humo, umekuwa ukilalamikiwa kwa muda mrefu, lakini hauchukuliwi hatua yoyote ukilinganishwa na kisiwani Unguja,
“Vyombo tunavyotumia kwa usafiri sisi Wapemba ni vya mizigo. Hakuna hatua zozote zinazochukuliwa, lakini vyombo vinavyofanya safari za Unguja kwenda Dar es Salaam, vinachekiwa kila mara” anasema Rashid.
Naye Mwajuma Omar wa shehia ya Kipangani wilayani Wete ambaye amepoteza watoto wanne na wajukuu wawili katika ajali hiyo, ameilalamikia serikali kwa kutokuwa makini katika ukaguzi wa vyombo vya usafiri,
“Ni kweli serikali itatupa mkono wa pole lakini hatuwezi kuwasahau watoto wetu. Nawashauri tu wawe makini katika kuvikagua vyombo vya usafiri” anasema.
Akisimulia tukio hilo, Mwajuma anasema kuwa watoto wake walikuwa katika meli hiyo na walimpigia simu kuwa wako njiani hadi saa tano usiku, lakini ilipofika saa nane usiku, walimpigia simu baba yao,
“Walipigia siku baba yao kuwa wanakufa, baada hapo hatukuwasikia tena hadi leo. Hatujafanikia hata kupata maiti” anasema.
Baadhi ya wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF) wamechukua hatua ikiwa ni pamoja na kuhakiki wananchi wao walioathiriwa na ajali hiyo. Hata hivyo kilio chao hakina tofauti na wananchi wao.
Mbunge wa jimbo la Ole, Rajab Mbarouk anasema kuwa serikali imeonyesha kuwatenga watu wa Pemba katika msiba huo.
“Tulitarajia viongozi wa serikali kuja huku Pemba kuomboleza na sisi. Lakini tunaona viongozi wote wameishia Unguja, hata hitima wameitolea huko, wakati wenye msiba tuko huku Pemba” anasema Mbarouk.
Mborouk ambaye amefanya tathmini ya wananchi wa jimbo lake waliofariki au kuptea katika ajali hiyo, anasema kuwa atapeleka hoja binafsi Bungeni ili kumwajibisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda,
“Inaonyesha serikali haina takwimu sahihi, ndiyo maana sisi tumeamua kufanya tathimini ya kina. Sisi ni wasemaji wa wananchi siyo serikali. Nina mpango wa kupeleka hoja binafsi Bungeni ili Waziri Mkuu awajibike” alisema Mbarouk na kuongeza,
“Nilishawahi kuuliza swali Bungeni kuhusu usalama wa vyombo vya majini lakini serikali haikuchukua hatua yoyote” anasema.
Mbunge wa jimbo la Ziwani Ahmed Ngwali anasema kuwa anafanya tathmini ya jimbo lake ili afanye utaratibvu wa kuishitaki serikali kutokana na uzembe uliosababisha ajali hiyo,
“Tukishapata orodha kamili ya wananchi, nakwenda kutafuta orodha ya abiria waliokuwa kwenye meli, nalinganisha. Kwa wale waliokuwa na tiketi, nitasimamia walipwe bima zao na mmiliki wa meli. Wale waliozidi nitaishitaki serikali kwa kuzembea” anasema Ngwali na kuongeza,
“Huu ni uzembe na ni lazima twende mahakamani. Ikiwa samaki wa Magufuli (Waziri wa Ujenzi) hadi leo wana wanasotesha watu mahakamani, itakuja kuwa watu?”.
Kwa upande wake Mratibu wa Wazee wa Pemba Ali Makame Issa anasema hadi sasa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, bado haijaonyesha sura yake halisi, kwahiyo siyo rahisi kuona matunda yake mapema,
“Unajua kwa sasa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, bado haijaonyesha sura yale halisi. Utakuta waziri ni wa CUF lakini watendaji wake wote ni wana CCM na bado wana zile chuki za kisiasa” anasema Issa.
Anamtetea Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano wa Zanzibar, Hamad Masoud Hamad, akisema kuwa tukio hilo linaweza kuwa njama kwake,
“Kwasababu yule waziri amechukua hatua mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuzuia meli ya Mv Maendeleo isifanye kazi kwakuwa ilikuwa na kasoro, akazuia Mv Serengeti na Sea Gull hadi zilipofanya marekebisho. Sasa kwa mlolongo huo, inawezekana watendaji wake tu, ndiyo wamefanya hujuma” anasema.
Issa anasema hata nahodha wa meli hiyo ambaye kwa sasa anatafutwa na jeshi la polisi, amepotea katika mazingira ya kutatanisha,
“Inatia shaka kuona kuwa jeshi la polisi linatangaza kumtafuta nahodha baada ya wiki moja, siku zote walikuwa wapi? Huenda wenyewe wanajua aliko” anasema.
Hata hivyo, akizungumzia ajali hiyo, Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano wa Zanzibar, Hamad Masoud Hamad anapinga kuwepo kwa njama wala uzembe katika ajali hiyo.
“Nasema ajali ni ajali, imeshatokea na kwa imani ya dini yangu, ni Mungu tu alipanga iwe. Hakuna njama yoyote iliyopangwa” anasema.
Akizungumzia kuwajibika kwake, Waziri Hamad ambaye anatoka chama cha Wananchi, (CUF) anasema yuko tayari kufanya hivyo ila hadi uchunguzi ufanyike kwanza.
“Mimi sihusiki na kukagua meli wala naibu waziri, kuna watendaji kama vile Wakurugenzi, Katibu, Naibu katibu na wengineo. Tusifanye mchezo wa ng’ombe ambapo anayekula ni wa mbele, lakini anapigwa bakora wa nyuma. Tusubiri uchunguzi ufanywe, ndiyo tutajua kama kuna uzembe au hujuma” anasema Hamad.
Hamad amesema kuwa hajakiangusha chama chake cha CUF kwakuwa tukio hilo limetokea kama ajali tu.
Lakini hisia hizo za Wapemba kutengwa na serikali hiyo, zimepingwa na Makamu wa kwanza wa serikali hiyo Seif Sharif Hamad akisema kuwa serikali hiyo imepanga kuwatembelea wote walioathiriwa na ajali hiyo.
“Nimekuja kuwajuli hali kutokana na ajali hii inayotugusa sote. Huu ni utaratibu tuliojiwekea, baada ya kutafakari suala hili, tumeona kwamba mimi nije kwanza, lakini viongozi wote watafika kuwajulia hali” anasema Maalim Seif.
Amekiri kuwepo kwa uzembe uliosababisha ajali hiyo na kusema kuwa serikali itafanya uchunguzi wa kina ili kubaini kasoro zilizokuwepo.
“Kuna kasoro zilizochangia ajali hiyo, kuna kasoro kwa wenye chombo, kuna kasoro kwa serikali hasa watu wenye dhamana hiyo, lakini hatutaki tuhukumu bila ushahidi. Tutafanya uchunguzi na matokeo yake yatawekwa hadharani kila mtu aone. Kama serikali au kama ni mtu yoyote awajibike.
Kuhusu jitihada za serikali ya Zanzibar, Maalim Seif anasema kuwa serikali hiyo kwa sasa ina mpango wa kuleta meli nyingine mpya ili kupunguza adha ya usafiri wa majini.
“Kwa sasa serikali ina mpango wa kununua meli mpya. Siyo hizi ‘boat’, tunataka meli zilizozoeleka na Wazanzibar. Mtu akitaka kuingia na mizigo yake na watu wake waingie kwa wingi” anasema Maalim Seif.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment