Thursday, August 4, 2011

AgriSol ni wawekezaji au wamekwenda kupora ardhi Mpanda?



AgriSol ni wawekezaji, au wamekuja kupora ardhi ya Mpanda?

Elias Msuya

KAMPUNI ya kimarekani ijulikanayo kama AgriSol Energy LLC inakamilisha taratibu za kumilikishwa na serikali ardhi ya hifadhi iliyopo katika wilaya ya Mpanda, mkoani Rukwa, uchunguzi umebaini.
Taarifa za awali zinaonyesha kuwa, ardhi inayotarajiwa kumilikishwa kwa kampuni hiyo inahusisha zilipo kambi za wakimbizi za Katumba yenye ekari 80,317 na Mishamo yenye ekari 219,800 na kambi ya Lugufu iliyoko mkoani Kigoma yenye ekari 25,000.
Mmoja kati ya washirika wa karibu wa kampuni hiyo nchini ni aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara Idd Simba ambaye ndiyo kiongozi wa Agrisol ya Tanzania yenye ofosi zake Mikocheni A Dar es Salaam. Mshirika mwingine nchini ni kampuni ya Serenge Advisers Limited” alisema Baha.
Katika waraka wake ambao Mwananchi imefanikiwa kuuona, Idd Simba anaitetea kampuni hiyo ya Marekani akisema kuwa taarifa zake zimekuwa zikipotoshwa na watu wengine,
“Habari za hivi karibuni zimekuwa zikipotosha nia yetu. Nikiwa kama mhusika wa Agrisol Tanzania tangu mwanzo najua watu, mipango, siasa na faida za mradi huu kwa Tanzania. Mradi wetu umelenga kuwashirikisha wakulima wa ngazi ya juu wa dunia na kuifanya ardhi ya Tanzania kuwa katika viwango vya juu na matumizi stahiki” anasema Idd Simba katika waraka huo.
Washirika wengine wa Agrisol ni pamoja na taasisi ya Pharos Global Agricultural Fund iliyo chini ya Pharos Financial Group ya Dubai inayoongozwa na Peter Halloran.
Nyingine ni Summit Group yenye makao makuu Iowa Marekani ikijishughulisha na kilimo na ufugaji na Chuo kikuu cha Iowa kinachoheshimika kwa masuala ya ardhi nchini humo. Chuo hicho kimepewa kazi ya kufanya upembuzi yakinifu ukiwamo wa udongo, hali ya hewa, mvua na hali ya eneo zima.
Tayari serikali imeshafanya makubaliano ya awali (Memorandum of understand) na kampuni hiyo.
Katika makubaliano hayo (tunao) Kuna mambo kadhaa yenye utata katika makubaliano hayo. Kwamfano malipo ya umilikishwaji wa ardhi hiyo ni madogo mno ambapo AgriSol Energy watatakiwa kulipa ada ya sh 200 na ushuru kwa halmashauri sh 500 kwa eka moja.
Vile vile wanamilikishwa eneo hilo kwa muda wa miaka 99 muda unaolalamikiwa na watu wengi kuwa ni mrefu mno.
Vilevile, kampuni hiyo kutumia wafanyakazi kutoka nje ya nchi hivyo kuwakosesha ajira wazawa.
Kampuni hiyo inayojihusisha na kilimo na ufugaji, kwa sasa inaishawishi serikali ibadilishe sera zake ili iruhusiwe kulima mazao yaliyorekebishwa viini tete (GMO).
Halafu kama kutatokea mgogoro, usuluhishi wake utakwenda kufanywa nchini Uingereza kwa sheria zao.
Nimezumza na Mkurugenzi wa wilaya hiyo Mhandisi Emmanuel Kalobero ambaye anakiri kuwepo kwa makubaliano hayo na kubainisha kuwa kampuni hiyo ilifika wilayani hapo na kuliona eneo lenyewe. Kisha ikawachukua baadhi ya maafisa wa wilaya hiyo na kuwapeleka Iowa Marekani ili kujionea yalipo makao makuu ya yake.
Anawataja maafisa hao kuwa ni pamoja na mkuu wa wilaya ya Mpanda Dk Rajab Rutenge, katibu tawala wa mkoa wa Rukwa Salum Chima, mwenyekiti wa Halmashauri ya Mpanda Philip Kalyalya, Makamu mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Sylvestre Swima, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Emmanuel Kalobero, Diwani na mjumbe wa kamati ya fedha Rose Malyalya, Diwani na mwenyekiti wa kamati ya maadili Teddy Nyambo, mwanasheria wa Halmashauri Patrick Mwakyusa, Afisa kilimo Fabian Kashindye na Haruna Mwalutanile.
Naye mwanasheria wa halmashauri ya Mpanda Patrick Mwakyusa, halmashauri hiyo ilipata agizo kutoka serikalini ya kuandaa maeneo husika kwaajili ya uwekezaji,
“Mnamo Februari mwaka 2010 tuliandikiwa kutoka mkoani tukiambiwa kuwa kuna mwekezaji (Agrisol) atakuja kuchukua maeneo ya makambi ya wakimbizi” anasema Mwakyusa na kuongeza,
“Maeneo hayo yalianza kukaliwa na wakimbizi tangu mwaka 1972 katika eneo la Katumba, mwaka 1978 wakimbizi wa Burundi waliokuwa Ulyanhulu walipozidi ndiyo wakahamishiwa eneo la Mishamo. Sisi kama Halmashauri hatuma maamuzi na maeneo hayo, tunapokea maelekezo tu”.
Mwakyusa anasema kuwa mwaka 2008, kampuni ya Agrisol ilikuja kufanya mazungumzo na serikali na mwaka 2010 kampuni hyo ilikuja wilayani humo kuangalia ubora wa udongo.
“Mazungumzo yalilenga kufanya utafitio na kuweka makubaliano kwamba uwekezaji utaanza baada ya serikali kuwaondoa wakimbizi, kufuatwa kwa sheria za ardhi na kwamba vijiji vya Watanzania vinavyozunguka kambi hizo vilindwe” anasema.
Anavitaja baadhi ya vijiji hivyo kati ya vingine 27 kuwa ni pamoja na Ndui Station, Laini, Kambuzi na Litapunga. Alisisitiza kuwa hata maeneo yenye shule za msingi na sekondari na zahanati hayataguswa.
Alisema kuwa mkataba rasmi utaingiwa Agosti mwaka huu na kwamba Halmashauri itafaidika kwa kutumia sheria za ushuru za ndani.
“Watakuwa wakilipa ushuru mara mbili kwa kila ekari ambapo ekari moja itakuwa ni sh 200 na ushuru wa sh500 kwa Halmashauri . Jamii zinazozunguka zitapata ajira, ujuzi na masoko ya bidhaa zao” anasema.
Kuhusu suala la muda wa mkataba, Mwakyusa anakiri kuwa hiyo ni changamoto watakayoizungumza wakati wa kusaini mkataba.
Kwa upande wake katibu tawala wa wilaya hiyo, Lauteri Kanoni anakiri kuhusishwa kwenye mkataba huo na kusemakuwa kampuni hiyo inajitosheleza kufanya uwekezaji mkubwa katika kilimo.
Anapinga suala la wafugaji kutoka mikoa mingine kuingiza mifugo wilayani humo akisema kuwa hawana utaratibu mzuri,
“Hatutaki kupokea mifugo kutoka nje ya mkoa huu. Tumeshafanya sensa na mifugo iliyopo inatosha. Eneo hilo tutawapa Agrisol kwasababu wana uwezo wa kuliendeleza, siyofugaji wasio na utaratibu mzuri” anasema.
Naye mkuu wa wilaya hiyo Dk Rajab Rutenge anasema kuwa hana wasiwasi na wawekezaji hao kwakuwa wataleta faida kubwa,
“Hatuna wasiwasi nao kwasababu wataleta faida kubwa. Mimi mtaalamu wa usalama wa chakula, Tanzania bado tuna uhaba wa chakula, tukiwaakila watu kama hao watazalisha chakula cha kutosha kumaliza tatizo la njaa” anasema.
Akizungumzia suala la mbegu zilizoboreshwa (GMO), Dk Rutenge anasema kuwa hilo pia siyo tatizo kwani tayari mazao hayo yalishaingizwa nchini tangu zamani,
“GMO siyo tatizo, mbona miaka ya 1980 tulikula unga wa yanga na Bulgur? Hizo si zilikuwa GMO? Nadhani suala la msingi ni kuwaelimisha wakulima. Vilevile wawekezaji hao wafuate sheria zetu” anasema Dk Rutenge.
Kwa mujibu wa tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Septemba 2010, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitembelea Marekani ambapo pamoja na mambo mengine alitembelea kampuni ya AgriSol Energy LLC yenye makao yake katika jimbo la Iowa
Lakini hivi karibuni suala hilo limeibuka Bungeni mjini Dodoma ambapo kambi rasmi ya upinzani Bungeni imehoji uwekezaji huo.
Akijibu hoja hizo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda anakiri mpango wa kuwamilikisha AgriSol eneo hilo akisema kuwa ni hatua ya kuimarisha uchumi wa mikoa ya Rukwa na Kigoma.
“Mimi natoka Mpanda na wananchi waliopo katika maeneo hayo ni wananchi wangu. Nikimsikia mtu anazungumzia suala hilo nashangaa, wale ni wapiga kura wangu” anasema na kuendelea,
“Kwa muda mrefu mikoa ya Rukwa na Kigoma imekuwa nyuma kwa kila kitu, si barabara ambapo lami inawekwa kwenye madaraja tu, hata kiuchumi. Tunalisha nchi nzima lakini hatuna kitu. Tulichofanya ni kuwarudisha wakimbizi kwao Burundi kwakuwa nchi yao sasa ina demokrasia. Sasa tunafanya nini kama kuna watu wanataka kuwekeza?”.
Waziri Mkuu Pinda anakanusha madai kuwa tayari kuna mkataba kati ya AgriSol na Halimashauri ya Mpanda, badala yake anasema kilichofikia ni makubaliano tu ya awali.
Ameongeza kuwa baada ya kufanya utafiti wa udongo, watalifikisha suala hilo kwenye kituo cha uwekezaji (TIC) na Wizara ya ardhi.
Wananchi wa Mpanda wanapinga
Licha ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuonyesha mzigo wa kuwatetea wananchi wake katika uwekezaji huo huku Halimashauri ya wilaya ya Mpanfa ikiutetea, wananchi wengi katika wilaya hiyo hawaelewi kinachoendelea na wengine wanaoelewa wanaipinga AgriSol.
Nimezungumza na mkuu wa kambi za wakimbizi za Katumba na Mishamo Athuman Igwe ambaye ameonyesha kuutilia shaka uwekezaji huo kwasababu mbili,
“Kwanza muda wa miaka 99 wanaopewa kumiliki ardhi yenyewe ni mrefu mno. Ni mkataba wa kikoloni, mambo yakiharibika itakuwa vigumu kujinasua.
Pili, ardhi yenyewe imechoka sana. Labda watumie mbolea nyingi kuiorutubisha. Au pengine kuna kitu wanakitafuta zaidi ya kilimo” anasema Igwe.
Naye diwani wa kata ya Litapunga yenye vijiji vya Kambuzi Holt, Litapunga na Ndui, Godfrey Lusambwa anasema kuwa ataupinga mkataba huo kwakuwa hakushirikishwa kama diwani,
“Huo uwekezaji nimeusikia kwenye vikao vya madiwani na tumeambiwa tuwahasishe wananchi. lakini kwenye vikao halisi vya makubaliano sikuhusishwa.kwamfano mkutano wa uwekezaji uliohudhuriwa na Waziri Mkuu Pinda aliyeisifia Agrisol, baadhi ya madiwani hatukuruhusiwa kuingia” anasema.
Naye afisa kilimo wa kata hiyo Righton Myombe alisema kuwa hawakuwahi kutangaziwa kuhusu uwekezaji wa eneo hilo,
“Siyo kweli kwamba serikali ilitangaza kwa wakulima kuhusu uwekezaji huo. Sisi tumeshukia tu Agrisol wamekuja na tunatakiwa tushirikiane nao, lakini hatujui faida yake” anasema.
Kwa upande wake mwanaharakati wa mazingira wilayani humo, Masanja Katambi anasema kuwa eneo hilo lilipaswa kugawiwa wafugaji ambao mara nyingi hutaabika kutafuta maeneo ya malisho.
“Mwaka 2009, tulikuwa na kikao na Waziri Mkuu Pinda kuhusu matatizo ya malisho kwa wafugaji, akatuahidi kutupatia eneo rasmi la kufugia. Tulitegemea kwamba wakimbizi wakiondoka tutapata eneo hilo. Sasa tumeshtushwa kuwa kuna Wamarekani wanakuja” anasema Katambi na kuongeza,
“Kwakweli ni janga la kihistoria, itakuwa kama mgodi wa Mwadui (William Diamondson) ambao mkataba wake haukomi hadi leo, wananchi hawaambulii kitu”.
Kwa upande wa kambi ya Mishamo, wanakijiji wanaozunguka kambi hizo nao hwaelewi watafaidikaje na mradi huo.
Afisa Mtendaji wa kata ya Mishamo Augustine Wangagwa anasema kuwa wananchi hawakushirikishwa kwa lolote katika uwekezaji huo, wamekuwa wakisikia sikia tu.
“Tumekuwa tukisikia tu huo uwekezaji, tulitarajia kushirikishwa kuanzia ngazi ya kitongoji. Lakini tunasikia mambo yaliishia kwenye halmashauri tu. Diwani wangu naye alisikia kwenye vikao lakini hakushirikishwa zaidi” anasema.
Hata hivyo Wangagwa anasema kuwa eneo hilo likiachwa baada ya kuondoka wakimbizi, halitatumika ipasavyo kwani wananchi katyika vijiji vinavyozunguka kambi hiyo ni 13,490 ukilinganisha na wakimbizi 58,000 waliopo katika kambi hiyo.
“Hatuna pingamizi, wao waje tu. Kwasababu hata wasipokuja eneo lote hili tutalifanyia nini? Sana sana tunachotaka kujua, tutafaidika nini?” anasema Wangagwa.
Naye Mbunge wa Mpanda Kati Said Arfi anasema kuwa atawasilsha hoja Bungeni kuupinga mkataba huo kwa madai kuwa ni batili.
“Nitawasilisha hoja binafsi katika bunge linalokuja, ili kuitaka serikali isitishe umilikishaji huo. Kama serikali itang’ang’ani, basi, iwatafutie AgriSol, ulinzi wa kutosha, kwani wananchi hawatakubali.
Anasema kuwa wanachokuja kufanya AgriSol ni kilimo cha nishati siyo mazao ya chakula.
“Kinacholengwa hapa ni kilimo cha nishati ya mimea (bio fuel). Hatari kubwa ninayoiona hapa ni kwamba watazalisha mazao hasa mahindi kwaajili ya kupata nishati na kulisha mifugo yao”.
Arfi anasema kuwa hajawahi kushirikishwa kwenye mikutano ya kuwajadili AgriSol, lakini atachukua hatua kwa manufaa ya taifa bila kujali mipaka ya jimbo.

Utata wa kuondoka wakimbizi
Pamoja na jitihada za serikali kuhakikisha kuwa eneo hilo linabaki wazi kwaajili ya kupewa mwekezaji, bado kuna utata wa kuondoka kwa wakimbizi hao.
Kwa mujibu wa Mkuu wa kambi hizo, Athuman Igwe, serikali ilikuwa imewapangia wakimbizi hao kuhamia katika mikoa 16, lakini wengi wamechagua kubaki mkoa wa Rukwa isitoshe wanapinga kulipwa kiasi cha 300,000 wakidai kuwa hakitoshi.
Katibu tawala wa wilaya ya Mpanda anasema kuwa Wakimbizi hao wanataka walipwe sh 2.8 milioni kwa kichwa.